Mbulu. Mkuu wa Wilaya ya Mbulu mkoani Manyara, Chelestino Mofuga amepiga marufuku raia wa kawaida kuajiriwa kwa kazi ya ulinzi bali shughuli hiyo wapatiwe askari wa jeshi la akiba la mgambo.
Pia, vijana wote wanaohitaji kujiunga na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) ni lazima wapite kwenye mafunzo ya mgambo.
Mofuga aliyasema hayo juzi kwenye uzinduzi wa mafunzo ya mgambo kwa wanafunzi 171.
Alisema atawachukulia hatua watakaoajiri raia wa kawaida kulinda ofisi, maeneo ya biashara, taasisi binafsi na za Serikali badala ya kuwatumia askari mgambo.
Mofuga alisema vijana wote wa Mbulu watakaotaka kujiunga na JKT ni lazima wapitie mafunzo ya mgambo ndipo waombe nafasi hiyo.
“Pamoja na hayo nawapongeza wananchi wa Mbulu kwa kuitikia wito wa vijana kujiunga kwa wingi kwenye mafunzo ya mgambo kwa ajili ya faida yenu,” alisema Mofuga.
Alifafanua kuwa kupitia mafunzo hayo, vijana wengi watanufaika nayo na wataweza kupata ajira mbalimbali tofauti na kabla ya kushiriki mafunzo hayo.
“Pia nachukua nafasi hii kwa kuwahamasisha wananchi wa Mbulu kujitokeza kwa wingi katika zoezi la kujiandikisha kupata vitambulisho vya Taifa,” alisema Mofuga.
Mmoja ya washiriki 171 wa mafunzo hayo, John Amnaay alimshukuru mkuu huyo wa wilaya kwa kukataza ajira za ulinzi kutolewa kwa raia wa kawaida.
“Tuna ari ya kushiriki mafunzo ya jeshi la mgambo na tunatoa ahadi ya kuzingatia masomo tutakayopatiwa na walimu wetu,” alisema.