F Serikali yakanusha kupokonya wafugaji mifugo | Muungwana BLOG
https://c2p.cleverwebserver.com/dashboard/6a0bec4b-79ba-11ef-ad2b-06f0639468d1

Serikali yakanusha kupokonya wafugaji mifugo

Naibu waziri mifugo na uvuvi Abdallah Ulega (Aliyevalia shati la rangi ya njano) akizungumza na wafugaji mkoani Tanga.

Serikali imewatoa  hofu wafugaji  nchini kuhusu  mchakato  wa  upigaji  chapa wa  mifugo  na kusema kuwa mpango huo haulengi kuchukua mifugo bali Serikali inataka kubaini  mifugo iliyopo.

Naibu Waziri  wa  Mifugo  na  Uvuvi, Abdallah  Ulega  ametoa hofu jana wakati akizungumza  na wakulima na wafugaji wa kijiji  cha  Perani  wilayani  Mkinga mkoa wa Tanga.

Kauli hiyo ya Ulega imekuja baada  wafugaji wa Perani kumweleza kwamba hawana elimu ya kutosha kuhusu mchakato huo na kwamba wanahisi kama mifugo yao inachukuliwa na Serikali .

Ulega  amesema Serikali ya Awamu ya Tano, ni sikivu na imedhamilia kuwatumikia vyema Watanzania na siyo kuwanyonya wananchi wa Taifa.

"Rais wetu ni mtu wa wanyonge, hakuna mtu yoyote atakayechukuliwa ngo'mbe zake.Bali tunataka  kujua mifugo yote iliyopo ili kuzuia mwingiliano na ile inayotoka nchi za jirani,"amesema  Ulega. 

Naibu waziri huyo, ametumia nafasi hiyo kuwasihi wafugaji na wakulima wa  eneo hilo kuacha mapigano baina yao kwani siyo jambo zuli na halileti taswira nzuri

"Naomba muishi kwa amani na utulivu kuanzia leo tatizo lenu nitalifikisha ngazi ya juu kuanzia kwa mkuu wa mkoa wa Tanga Martine Shigela  ili atume wataalamu waje kuangalia namna ya kusimamamia  vyema mpango kazi,"amesema Ulega.

Awali mwenyekiti wa kijiji hicho, Letinga Oyaya alimweleza naibu waziri huyo kwamba wanaomba kuelimishwa namna ambayo mchakato wa upigaji chapa utakavyotekelezwa na madhumuni yake.