F Sethi aendelea kuteswa na puto tumboni | Muungwana BLOG
https://c2p.cleverwebserver.com/dashboard/6a0bec4b-79ba-11ef-ad2b-06f0639468d1

Sethi aendelea kuteswa na puto tumboni

Dar es Salaam. Wakili  Alex Balomi ameieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuwa mshtakiwa Harbinder Sethi licha ya kupelekwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili na kuchukuliwa vipimo hadi sasa bado hajapa majibu wala matibabu yoyote na afya yake inazidi kudhoofika.

Ameeleza hayo leo Ijumaa mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi mara baada ya Wakili wa Serikali  Mwandamizi, Kishenyi Mutalemwa kudai upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika na akaomba ipangiwe tarehe nyingine.

Kishenyi baada ya kueleza hayo, Wakili Balomi alieleza kuwa kwa kiasi fulani upande wa mashtaka umetekeleza amri ya Mahakama kwa kumpeleka Muhimbili na kuchukuliwa vipimo lakini hajapewa majibu na wala hajatibiwa hadi sasa.

Ameeleza kuwa lile puto alilowekewa tumboni Sethi linatakiwa kubadilishwa mwishoni kwa mwezi huu, lisipobadilishwa litageuka kuwa sumu na kuhatarisha uhai wake.

Amesema daktari aliyechukua vipimo ampatie majibu ili aweze kujua hali ya afya yake ikoje.

Wakili Kishenyi baada ya kutolewa kwa maelezo hayo amesema kuwa wao wamekwishatekeleza  amri ya mahakama, hawana cha kufanya zaidi kwa sababu majibu ni siri ya magonjwa na daktari.

Mwendesha Mashtaka Mwandamizi wa Takukuru, Leonard Swai yeye naye ameeleza kuwa suala la majibu ni suala la magonjwa na daktari.

Baada ya kutolewa kwa maelezo hayo, Hakimu Shaidi amesema amri ya Mahakama imetekelezwa ambapo mshtakiwa alipelekwa Muhimbili na siyo jukumu la Mahakama kuingilia kazi ya daktari hivyo alishauri mawakili wa upande wa utetezi wafuate utaratibu.

Kesi imeahirishwa hadi Novemba 10, 2017 kwa ajili ya kutajwa na kuusisitiza upelelezi ukamilishwe.