Mchezo huu unatarajiwa kuwa na ushindani wa hali ya juu kutokana na timu hizo kuwa katika nafasi sawa ya msimamo wa ligi licha ya Simba kuongoza kwa idadi ya mabao ya kufunga, huku kila moja ikihitaji kukaa kileleni.
Mechi hii inatarajiwa kuwa ni ya vita na kisasi kutokana na hali jinsi ilivyo katika mechi husika ambapo kila upande utahitaji kufanya vyema.
Yafuatayo ni baadhi ya mambo ambayo yanatarajiwa kuifanya mechi hiyo kuwa ni ya vita na kisasi.
Imekaa vibaya kwa upande wa makocha wa timu zote mbili, kutokana na historia za timu hizo ambapo mara nyingi makocha wamekuwa wakifungashiwa virago vyao pale wanapofungwa na wapinzani wao.
Hivi karibuni kulizuka uzushi juu ya Yanga kutaka kumuondoa kocha wake, George Lwandamina kutokana na matokeo mabaya katika mechi za awali jambo ambalo uongozi wa klabu hiyo ulikanusha, lakini waswahili husema lisemwalo lipo, hivyo mechi hiyo inaweza kuwa katika wakati mgumu kwa upande wake.
Vilevile kwa upande wa Simba, Kocha Joseph Omog amekalia kuti kavu kwa muda mrefu kutokana na uongozi wa klabu hiyo kutaka kumuondoa kutokana na madai ya kutokifundisha vyema kikosi hicho kwa kuona kuwa kimemzidi uwezo, lakini mkataba aliosaini umeonekana kumbeba kutokana na baadhi ya vipengele kuwabana waajili wake.
Hivyo basi, mechi hii ndiyo itakayotoa maamuzi juu ya kuendelea kuwepo katika kikosi hicho kwa kuwa inadaiwa kuna kipengele alichosaini kinaeleza kuwa iwapo t i m u haitaongoza msimamo wa ligi, itawapa nguvu viongozi kuweza kuvunja kandarasi hiyo.
Mshambuliaji wa Simba, Haruna Niyonzima akiopambana na wachezaji wa Simba.
Hivyo, atakuwa na kibarua kigumu kuhakikisha anafanikiwa kushinda mchezo huo ambao utakuwa na upinzani mkubwa.
KILA TIMU ITAHITAJI KUKAA KILELENI
Simba na Yanga zimefungana katika msimamo wa ligi kutokana na zote kuwa na pointi 15, huku Simba ikiongoza kwa kuwa na idadi kubwa ya mabao ya kufunga. Simba ina mabao 19 na Yanga ina mabao 10.
Hivyo, kutokana na jinsi msimamo ulivyo, timu ambayo itashinda katika mchezo huo ndiyo itakayopata nafasi ya kuongoza msimamo wa ligi na iwapo itatokea wakatoa sare na Mtibwa Sugar yenye pointi 15 ikishinda mechi yao ya Jumapili dhidi ya Singida United basi itakaa kileleni.
KUONYESHANA UBORA WA VIKOSI
Kila timu inajinadi kuwa na kikosi bora ambacho imekisajili msimu huu, hivyo mashabiki wanasubiri kwa hamu kubwa kuona timu gani itaonyesha ufundi zaidi katika mchezo huo.
AJIBU, NIYONZIMA & OKWI VIVUTIO
Kwa sasa habari ya mjini katika timu hizo ni kuhusiana na viwango vya wachezaji Ibrahim Ajibu wa Yanga na Haruna Niyonzima na Emmanuel Okwi wa Simba, hivyo kila mmoja atahitaji kuona wanafanya nini katika mechi hiyo ya kesho.
Kwa upande wa Okwi, ndiye mchezaji kinara wa mabao kwenye ligi akiwa na mabao nane ambayo yameifanya kikosi hicho kukaa kileleni kwa tofauti ya mabao.
Aidha, wachezaji Ajibu na Niyonzima, kwa sasa ni gumzo kutokana na viwango wanavyoonyesha. Mashabiki wa timu hizo wamekuwa wakirushiana maneno huku wale wa Yanga wakidai Simba wamepoteza mchezaji (Ajibu) kwani amekuwa muhimu Jangwani na Niyonzima akipondwa kwa kuonyesha uwezo wa kawaida tofauti na ule aliokuwa akionyesha Yanga.
HOFU YA MASHABIKI
Hofu kubwa ya mashabiki kuelekea mchezo huo, itakuwa namna ya kuingia uwanjani kwani kwa muonekano wa haraka Uwanja wa Uhuru jinsi ulivyo hauwezi kukidhi mahitaji ya mashabiki kutokana na udogo wa uwanja huo tofauti na ule wa Taifa ambao ni mkubwa.
Kuna uwezekano mkubwa kwa mashabiki wengi kuangalia mpira huo kupitia runinga kutokana na kushindwa kuingia uwanjani licha ya kuhitaji kuwaona wachezaji ‘live’ uwanjani.