F Wabunge waibua hoja hii | Muungwana BLOG
https://c2p.cleverwebserver.com/dashboard/6a0bec4b-79ba-11ef-ad2b-06f0639468d1

Wabunge waibua hoja hii

Dodoma.Hoja ni kiongozi gani kati ya wabunge, wakuu wa wilaya na mikoa ni mkubwa kwa cheo imeibuka kwenye semina ya wabunge mjini Dodoma.

Hoja hiyo imeibuka leo Jumapili Oktoba 29,2017 katika semina ya wabunge wa kamati mbili za Bunge kuhusu masuala ya kidiplomasia na itifaki.

Semina hiyo imeandaliwa na Bunge kupitia mradi wa kujengea uwezo wabunge na wawakilishi unaofadhiliwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Maendeleo (UNDP).

Washiriki wa semina ni wajumbe wa Kamati ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama; Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC) na wawakilishi kutoka vyama vya kibunge.

Akizungumza katika majadiliano, Mbunge wa Sumbawanga Mjini (CCM), Aeshi Hillal ametoa mfano wa ziara za kikazi akisema mbunge huwekwa wa mwisho, akitanguliwa na mkuu wa mkoa na mkuu wa wilaya.

“Unakuta mkoa katika ziara gari la mbele yupo RC ameweka bendera, linalofuatia ni la DC naye ameweka bendera na la mbunge linakuwa nyuma. Tunaomba utufafanulie katika hilo,” amesema.

Katika hilo, Mbunge wa Morogoro Kusini-Mashariki (CCM), Omary Mgumba amesema mkuu wa wilaya anamwakilisha Rais na katika wilaya nyingine huwa zina majimbo mawili ya uchaguzi, hivyo kumfanya mbunge kuwa na eneo dogo la kiutawala ikilinganishwa na mkuu wa wilaya.

“Siku zote ukweli ni mchungu na hasa ukiwa hutaki kuusikia. Utakuta wilaya moja ina majimbo mawili, mbunge wa jimbo moja utawala wake ni kwenye jimbo lake tu lakini mkuu wa wilaya ni mtawala katika majimbo yote mawili yaliyo katika wilaya yake,” amesema.

Akizungumzia hilo, Mbunge wa Mtambile (CUF), Mosoud Abdallah, amehoji itifaki inazungumzaje kuhusu mbunge wa jimbo na wa viti maalumu wanapokuwa jimboni.

“Tunapokuwa jimboni ni mbunge gani anakuwa mkubwa kwa cheo kati ya mbunge wa viti maalumu na wa jimbo,” amehoji.

Akijibu hoja hizo, ofisa kutoka Wizara ya Mambo ya Nje, Kitengo cha Uhusiano wa Kimataifa, Ally Masabo amesema kiitifaki mkuu wa mkoa ndiye mwenye mamlaka katika mkoa, hivyo ndiye anayetakiwa kuwa mbele katika msafara mkoani.

"Suala hili wabunge wana wajibu wa kuangalia, na utatuzi upo kwenu wabunge," amesema Masabo ambaye ametoa mada katika semina hiyo.

Mwananchi: