MAHAKAMA ya Wilaya ya Dodoma, imewahukumu wakazi wawili wa Dodoma kifungo cha miaka 20 jela kila mmoja kwa kosa la kukutwa na nyara za serikali.
Waliohukumiwa ni Jumanne Mlaga na Alfred Nyagawa ambao walikutwa na bunduki moja na meno mawili ya tembo na mifuko yake
kinyume cha sheria ya wanyamapori.
Akisoma hukumu hiyo jana, Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama hiyo, James Karayemaha, alisema imewatia hatiani kutokana na kosa hilo ambalo walilifanya Aprili, 2016.
Alisema katika kesi hiyo upande wa mashtaka uliwasilisha mashahidi sita na vielelezo tisa ambavyo vimewatia hatiani washtakiwa hao.
Pia alisema washtakiwa kutokana na kutiwa hatiani, wamehukumiwa kwenda kutumikia adhabu hiyo na kwamba kama hawajaridhika, wana haki ya kukata rufani.
Alipongeza jitihada za mawakili kusimamia masuala ya ujangili jambo ambalo linachangia kupunguza wahalifu kwa upande wa maliasili na hifadhi zake.
Hakimu alisema mahakama imetoa adhabu hiyo ili iwe fundisho kwa wengine ambao wanajihusisha na
biashara hiyo haramu.
Alisema pamoja na adhabu hiyo, pia mahakama imetaifisha bunduki moja na meno ya tembo waliyokutwa nayo.
Kabla ya kutolewa hukumu hiyo, wakili wa washtakiwa hao, Magiri Mbasha, aliiomba mahakama iwapunguzie adhabu kwa sababu washtakiwa wana wazazi wanaowategemea.
Hata hivyo, Hakimu Karayemaha alisema hakuna sababu ya kuwapunguzia adhabu kwa sababu kila Mtanzania ana wazazi na familia ambazo zinawategemea, hivyo adhabu hiyo ni stahiki kwao kwa sababu wamelisababishia taifa hasara kubwa kwa kuwa tembo wengi wanapotea.
Kwa pande wake, Wakili wa Serikali, Salim Msemo, alidai vitendo vya ujangili vimesababisha tembo kupungua kwenye hifadhi mbalimbali kutoka asilimia 60 hadi 40.
Alidai kuwa adhabu hiyo inawastahili na mahakama itoe adhabu ambayo itakuwa fundisho kwa sababu wamekuwa wakitumia wanyamapori kujinufaisha na familia zao badala ya serikali kunafaika.