Waziri wa Maliasili na Utalii, Mh. Hamisi Kigwangalla amefunguka na kuwapa siku saba wavamizi ambao wapo kwenye pori tengefu la Loliondo kuondoka mara moja ndani ya siku hizo kwani wasipofanya hivyo baada ya hapo mali zao zitataifishwa na serikali.
Kigwangalla amesema uwepo wa wavamizi hao ambao wana ng'ombe zaidi ya 6,000 na matrekta zaidi ya 200 kutoka nchi ya jirani imekuwa sababu kubwa ya chanzo cha mgogoro wa ardhi baina ya vijiji na hifadhi hiyo.
"Kuna taarifa kwenye eneo lenye mgogoro la Pori Tengefu la Loliondo, kuna ng'ombe zaidi ya 6,000 na trekta zaidi ya 200 toka nchi jirani, yote kinyume cha sheria! Uwepo wao siyo tu unahatarisha uhai wa mfumo wa ikolojia ya Serengeti-Mara, bali pia unapunguza eneo la kuchungia kwa wenyeji wa Loliondo. Hivyo kuleta kiu ya wananchi wa Loliondo kuingia ndani zaidi ya eneo la hifadhi kutafuta malisho na hatma yake kuhatarisha uhai wa Serengeti. Uvamizi huu wa wenzetu kutoka nchi jirani ni moja ya sababu kubwa (zilizojificha) za mgogoro wa ardhi baina ya vijijj na hifadhi kukolea moto" alisema Waziri Kigwangalla
Aidha Waziri huyo amesema wakati wanaendelea kutafuta ufumbuzi wa kudumu wamewataka wavamizi hao kuondoka katika maeneo hayo
"Wakati tukiendelea kutafuta suluhisho la kudumu, tutaondoa makando kando kama haya haraka. Leo tumetoa siku saba kwa wavamizi wote toka nchi jirani waliopo eneo la Loliondo bila kufuata taratibu za kisheria waondoke na mali zao la sivyo tutazitaifisha" alisisitiza Kigwangalla.