Zanzibar/Tanga. Polisi Zanzibar imesema imepokea taarifa ya kuzama kwa boti katika Bahari ya Hindi iliyokuwa ikitokea Tanga kuelekea Kisiwa cha Pemba.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kaskazini Pemba, Haji Khamis Haji akizungumza na MCL Digital leo Alhamisi Novemba 30,2017 amesema wamepokea taarifa leo asubuhi kutoka kikosi cha KMKM ambacho ndicho chenye dhamana ya kufanya msako na doria katika Bahari ya Hindi eneo la Zanzibar. Amesema wanaendelea na ufuatiliaji .
“Wenzetu wa KMKM wameanza utafutaji wa boti hiyo ambayo hatuijui jina wala ilikuwa na kitu gani na idadi ya watu waliokuwamo,” amesema.
Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, Leon Rwegasira amesema boti hiyo ilikuwa na watu watano akiwamo nahodha na ilikuwa imebeba mifuko 900 ya saruji ikitokea Tanga kuelekea Zanzibar.
Ofisa wa Mamlaka ya Udhibiti Usafiri wa Majini na Nchi Kavu (Sumatra) Mkoa wa Tanga, Dk Walukani Kulyamba amesema taarifa kamili zitatolewa zitakapothibishwa.
Awali, Shirika la Habari la AFP lilisema watu tisa hawajulikani waliko baada ya boti waliyokuwa wakisafiri kuzama katika Bahari ya Hindi.
Shirika hilo limesema boti hiyo ilikuwa ikisafirisha vifaa vya ujenzi ikiwemo saruji na ilikuwa na wafanyakazi watatu na abiria sita.
Source: Mwananchi