Harare, Zimbabwe. Viongozi wa chama tawala cha Zanu PF wanakutana leo kuandaa rasimu ya uamuzi wa kumwondoa madarakani Rais Robert Mugabe mwishoni mwa wiki hii.
Pia, wataandaa mazingira ya kumfungulia mashtaka wiki ijayo ikiwa ataendelea kukataa kuachia madaraka, kiongozi wa ngazi ya juu amesema.
"Hakuna kurudi nyuma," kiongozi huyo aliliambia shirika la habari la Reuters. "Ikiwa atazidi kuwa mkaidi, tutaandaa mazingira ili afukuzwe Jumapili. Hilo likifanyika atafunguliwa mashtaka Jumanne."
Hatima ya Mugabe bado haijulikani hadi leo kwani imeelezwa amekataa juhudi zote za kumtaka ajiuzulu baada ya jeshi kutwaa mamlaka ya nchi ambalo hadi wiki hii lilikuwa nguzo muhimu katika utawala wake wa miaka 37.
Jeshi lilisema kupitia televisheni ya taifa kwamba lilikuwa linafanya mazungumzo ili kupata ufumbuzi na kwamba litaliarifu taifa kuhusu matokeo haraka iwezekanavyo.
Marekani, mkosoaji wa miaka mingi wa Mugabe kuhusu ukiukwaji wa haki za binadamu na wizi wa uchaguzi inataka “enzi mpya” Zimbabwe, alisema ofisa wa ngazi za juu wa mambo ya nje wa Marekani kuhusu masuala ya Afrika ukiwa ni wito uliowazi wa kumtaka mzee huyo aondoke.
Mkanganyiko umejitokeza pale Mugabe alipoonekana jijini Harare kwenye picha akiwa mtu mwenye tabasamu na akisalimiana na mkuu wa majeshi wa Zimbabwe, mtu ambaye yuko nyuma ya mapinduzi na kuibua maswali kuhusu kukaribia mwisho wa enzi zake.
Katika hali isiyotarajiwa Mugabe aliondoka kwa msafara kwenye nyumba yake ya kifahari maarufu kama "Paa la Bluu" alikokuwa amezuiliwa na jeshi na akaenda hadi Ikulu ambako alipigwa picha zilizosambabzwa kwenye vyombo vya habari alikutana na mkuu wa majeshi, Jenerali Constantino Chiwenga na wapatanishi kutoka SADC.