F Sikukuu ya Krismasi kuwa chungu kwa Wakazi wanaokabiliwa na Bomoabomoa | Muungwana BLOG
https://c2p.cleverwebserver.com/dashboard/6a0bec4b-79ba-11ef-ad2b-06f0639468d1

Sikukuu ya Krismasi kuwa chungu kwa Wakazi wanaokabiliwa na Bomoabomoa


Dar es Salaam. Wakati sikukuu ya Krismasi ikikaribia, hali si shwari kwa wakazi wa Ubungo hadi Kimara ambao nyumba zao zimewekwa alama ya X zinazotarajiwa kubomolewa Desemba 21.

Nyumba 450 kati ya 1,200 zilizo ndani ya mita 91 katika hifadhi ya barabara zitabomolewa mwezi ujao kupisha upanuzi wa barabarahiyo ya Morogoro.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti, wakazi wa maeneo hayo walisema sikukuu ya mwaka huu itakuwa chungu kwao tofauti na miaka mingine ambayo walisherehekea wakiwa kwenye nyumba zao.

Mkazi wa Ubungo eneo la Kibo, Aloyce Chitala alisema sikukuu haitakuwa nzuri kwa upande wake kwa kuwa mwisho wa kuwapo kwenye nyumba yake ni Desemba 20 kwa mujibu wa barua aliyopewa na Wakala wa Barabara (Tanroads).

“Barua inatutaka tuondoke mwezi ujao, kwa hiyo hata ile shamrashamra ya sikukuu mwaka huu itakuwa ngumu, fikiria sasa hivi tumeambiwa tubomoe unafikiri baada ya kubomoa hapa kuna sikukuu tena zaidi ya simanzi?” alihoji.

Chitala alisema wanatambua kuwa ubomoaji huo ni kwa ajili ya maendeleo, lakini bado wanahitaji kulipwa chochote kwa ajili ya kutafuta sehemu nyingine ya kujisitiri bila hivyo yatawakuta kama ya Kimara ya kulala nje.

Alisema wakati wenzao wa Kimara Stop Over wanabomolewa nyumba zao, wao walijua wamepona, lakini hali ni tofauti na hatimaye maumivu yameangukia katika kipindi cha sikukuu.

“Inauma mtu unaishi miaka mingi halafu nyumba inakuja kubomolewa tena kwa kupewa mwezi mmoja pekee, basi wangesogeza mbele angalau hii sikukuu ipite ili na sisi tufurahi kama wenzetu,” alisema.

“Wakati huo nyumba zenyewe zitakuwa zimeshavunjwa na wengine tunaishi nje hivyo hakuna sikukuu tena, wenzetu wenye furaha tunawatakiwa kila la kheri katika sikukuu hii.”

Mkazi mwingine wa hapo, Idd Vagi alisema ni kweli eneo ni la Serikali, lakini awali wananchi hawakushirikishwa kwa kupewa elimu ili wasijenge.

Vagi mwenye umri wa miaka 75 alisema amekuwa akiishi sehemu hiyo tangu mwaka 1970 wakati huo eneo hilo likiwa pori.

“Walikuja hapa mwezi uliopita wakatoa notisi, wakasema tuanze kubomoa ndani ya mwezi mmoja kinyume na hapo inabidi tuwalipe kama wakija kubomoa wenyewe,” alisema.

Mzee huyo alisema wananchi wanaosomesha utakuwa ni mwezi mbaya zaidi kwao kwa kuwa watoto wanahitaji sare za shule na ada huku nyumba zao zitakuwa zinabomolewa.

“Ni kweli mwezi huu sikukuu sio nzuri hasa kwa wenzetu, lakini tutafanyaje hatuna jinsi ndiyo Serikali yetu hii, hatuna pa kwenda na hatuna cha kufanya tupo tu,” alisema.

Vagi aliongeza kwamba suala la kuhama sio gumu, lakini kuhamisha vitu ikiwamo matofali na vifaa vingine ni vyema Serikali ikawapatia fidia kidogo ili wapate fedha za kusafirishia mizigo yao kwenda sehemu nyingine ili kupisha iendalee na ujenzi.

Bernadeta Mushi ambaye ameanza kubomoa nyumba yake, alisema kwa sasa hajui sikukuu itakuwaje kwa upande wake kwa kuwa hadi hafahamu mahali atakakokwenda kuishi baada ya nyumba yake kubomolewa.

Alisema baada ya kupata notisi iliyomtaka kuondoka ndani ya mwezi mmoja alichanganyikiwa.

Hata hivyo, alisema anachokifanya kwa sasa ni kutoa vyombo vyake ili kama nyumba yake itabomolewa visiharibike.

“Yaani dada kwa sasa ukiniuliza kuhusu sikikuu sijui hata nijibu nini kwani navuta picha siku hiyo nitakuwa hospitali au chini ya mti maana sina pa kwenda,” alisema.

Akizungumzia hali hiyo, meya wa Manispaa ya Ubungo, Boniface Jacob alisema hadi nyumba 450 zimeshawekwa alama ya X na mwezi ujao zitabomolewa.

Alisema wananchi wana maumivu kwa kuwa wanatakiwa kuondoka mwezi huu bila malipo, hali inayosababisha hofu miongoni mwao ya kukosa makazi.

“Kwa kweli hivi sasa hali ni mbaya kwa wananchi hawa ambao wanatakiwa kuondoka. Utata ni kwamba kuna wenzao ambao walilipwa, kwa hiyo nao wanadai malipo yao,” alisema.

Akizungumza kwa simu na mwandishi wa habari hizi, meneja wa Tanroads Mkoa wa Dar es Salaam, Julius Ndyamkama alisema ubomoaji utaanza rasmi Desemba kwa wale waliowekewa X mwezi huu.


  1. Hata hivyo, hakutaka kuingia kwa undani kuhusu suala hilo.