Kilimanjaro Stars leo watacheza na Zanzibar Heroes katika michuano ya Chama cha soka Afrika Mashariki na kati (CECAFA) yanayofanyika nchini Kenya majira ya saa nane mchana, nani kubuka mshindi leo?
Kocha mkuu wa timu ya taifa ya Tanzania bara maarufu kama Kilimanjaro Stars amesema wanaingia uwanjani wakiwa na hofu kubwa kwa kiwango walichoonesha Zanzibar katika mchezo wao wa awali.
"Tunaingia katika mchezo mgumu kwetu, tumejiandaa vizuri ili kupata alama tatu kujihakikishia nafasi ya kusonga mbele katika hatua inayofuata" , Ammy Ninje amesema
Kwa upande wa kocha mkuu wa Zanzibar Heroes amesema ni mchezo wa kihistoria hivyo watajitahidi wapate matokeo mazuri.
"Ni mchezo wa kihistoria kwetu sio rahisi kutabiri, lengo letu kushinda, kila mmoja ana mawazo hayo" , amesema Hemed Morocco
Timu mbili katika kundi "A" zitakazopata alama za juu zitapata nafasi ya kusonga mbele, kundi hilo lina timu tano ikiwemo wenyeji Kenya, Kilimanjaro Stars, Zanzibar Heroes, Libya na Rwanda.
Mchezo huu utakuwa mkali na mgumu pande zote kutokana na wachezaji wengi wa timu hizo kujuana na wengi wao kucheza ligi kuu Tanzania bara.