Jukwaa la Katiba Tanzania (Jukata) limesema litafungua kesi ya kupinga katazo maandamano wakati wowote kuanzia sasa.
Jukwaa hilo limesema kesi hiyo itafunguliwa na Mkurugenzi wa Chama cha Wanasheria Watetezi wa Mazingira (Leat), Dk Lugelemeza Nshala ambaye ataongoza jopo la mawakili 10.
Mkurugenzi wa Jukata, Hebron Mwakagenda alisema jana kwa simu kuwa wameshakusanya ushahidi wa kutosha wa kuishtaki Serikali kwa kuzuia maandamano.
“Kikubwa katika mwaka huu ni kufungua kesi ya kupinga katazo la maandamano, maana ni kama yamefutwa kiaina hivi. Tumeshazungumza na wakili Dk Lugelemeza Nshala amekubali na ataongoza mawakili wengine 10 katika kesi hiyo,” alisema Mwakagenda.
“Tumekusanya ushahidi wa kutosha, ukiwemo wa sisi wenyewe. tuliomba kufanya maandamano Polisi tukakataliwa kwa sababu zisizo na kichwa wala miguu. Tukaomba tena tukakataliwa, huo ni sehemu ya ushahidi wetu.”
Alipoulizwa kuhusu mpango huo, Dk Nshala alisema upo lakini bado maandalizi hayajakamilika.
“Ni kweli kuna hiyo kesi lakini bado hawajafanya chochote mpaka sasa,” alisema.
Katazo la shughuli za siasa lilianza kutolewa na Jeshi la Polisi Novemba 6, 2015 likipiga marufuku maandamano na mikutano ya vyama vya siasa iliyokuwa imepangwa kufanyika kwa nyakati tofauti kwa madai ya kuwapo hali tete ya kisiasa.
Aliyekuwa msemaji wa polisi wakati huo, Advera Bulimba alisema vyama vya CCM na Chadema tayari vilikuwa vimeshawasilisha maombi ya kufanya mikutano na maandamano sehemu mbalimbali hapa nchini.
Januari 23, 2016, Rais John Magufuli mwenyewe alitangaza kusimamisha shughuli za siasa ikiwa pamoja na mikutano na maandamano, alipokuwa akipokea ripoti ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 kutoka kwa Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), wakati huo, Jaji Damian Lubuva.
Rais Magufuli aliwataka wanasiasa wa upinzani kufanya siasa baada ya miaka mitano ili apate nafasi ya kutekeleza ahadi alizowaahidi Watanzania.
Aidha, Julai 29, 2016 Rais Magufuli akiwa katika ziara mkoani Singida aliwaonya wanasiasa wanaotaka kuleta vurugu akisema hajaribiwi.
Onyo hilo lilikuja wakati Chadema ikiwa imetangaza kufanya maandamano nchi nzima yaliyopewa jina la Umoja wa Kupinga Udikteta Tanzania (Ukuta).
Awali, maandamano hayo yalipangwa kufanyika Septemba Mosi, 2016 lakini yaliahirishwa kwa mwezi mmoja kabla ya kufutwa.