Kitendo cha Tanesco kuikatia Dawasco umeme, kwazua taharuki

Deni la zaidi ya Sh25 bilioni ambalo Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) linalidai Shirika la Majisafi na Majitaka Dar es Salaam (Dawasco) jana lilizua kizazaa cha upatikanaji wa maji kwa muda jijini hapa na baadhi ya maeneo ya Mkoa wa Pwani.

Kizaazaa hicho kimetokana na jana mchana Tanesco kukata umeme kwa saa kadhaa katika mitambo ya Dawasco ya Ruvu Chini na Ruvu Juu kutokana na deni hilo lililotajwa kuwa linatokana na malimbikizo ya nyuma.

Baada ya taarifa za kuzimwa kwa mitambo ya umeme kuanza kusambaa, jioni Dawasco ililipa benki kiasi cha Sh2 bilioni huku kiasi kingine kama hicho ikiahidi kulipa kabla ya Ijumaa hivyo Tanesco kurejesha umeme.

Kukatwa kwa umeme katika mitambo hiyo kulizua hofu kwa wateja zaidi ya 200,000 wa Jiji la Dar es Salaam, Mlandizi na Bagamoyo waohudumiwa na mitambo hiyo.

Machi 5 mwaka jana, Rais John Magufuli wakati akizindua kituo cha kupooza umeme cha Tanesco mjini Mtwara, alitoa maagizo kwa shirika hilo kuwakatia umeme wateja wote wenye madeni bila kujali kama ni taasisi ya umma au binafsi.

Tanesco walikata umeme Dawasco ikiwa ni utekelezaji wa agizo ililolitoa Januari 11 kwa wadaiwa wake sugu, ikiwataka wawe wamelipa madeni wanayodaiwa ndani ya siku nne kabla ya jana.

Akizungumza na Mwananchi jana kabla ya umeme kurejeshwa, Kaimu Mkurugenzi wa Tanesco, Dk Tito Mwinuka alisema operesheni hiyo ya kuwakatia umeme wateja sugu itakuwa endelevu.

“Kazi hii hatujaianza leo (jana) tunaendelea nayo, lazima wadaiwa wote sugu watulipe madeni tunayowadai, ila ukiniuliza ni nani na nani wanaodaiwa na wameshakatiwa, jibu sina,” alisema Dk Mwinuka na kuongeza;

“Kama mmesikia watu wanasema yamewakuta, basi wafuateni wao watawaambia kilichowakuta ila siwezi kuwataja wateja wetu kwa majina. Huduma tunayoitoa sisi ni sawa na daktari na mgonjwa na daktari haruhusiwi kutoa siri za mgonjwa wake.”

Bila kufafanua kiasi kilicholipwa, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Dawasco, Cyprian Luhemeja alisema umeme umerejeshwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji na Umwagiliaji, Profesa Kitila Mkumbo alisema aliwaagiza Dawasco kukutana na Tanesco ili kujadiliana jinsi ya kulipa deni hilo

“Nimewaagiza Dawasco na Tanesco wakae wajadiliane walipe deni hilo haraka kesho (leo) ili huduma zirudi na wananchi wapate maji kwani deni hilo haliwahusu na wanapaswa kupata huduma ya maji kama kawaida,” alisema Profesa Mkumbo.

Chanzo kutoka Tanesco kililidokeza Mwananchi kuwa ‘baada ya kukatiwa umeme, kiasi hicho cha fedha kilipwa.“Kesho (leo) watalipa Sh500 milioni na Ijumaa watalipa Sh500 milioni lakini sisi (Tanesco) lengo letu wangepunguza deni kwa kiwango kikubwa.”

“Kuna (anamtaja kigogo wa wizara ya nishati) ameingilia kati kutokana na kupigiwa simu na watu wengi kuhusu tatizo la maji hasa maeneo ya Pwani hivyo kuagiza yarudishwe na deni hilo lilipwe haraka.”