Hatimaye mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe ametuliza mtifuano ulioibuka miongoni mwa wanachama wake baada ya waziri mkuu wa zamani, Edward Lowassa kufanya kikao cha faragha na Rais John Magufuli.
Pia mwenyekiti huyo wa chama hicho kikuu cha upinzani amesema Chadema haitakubali kuchonganishwa kutokana na kikao hicho cha viongozi hao wawili.
Mbowe alisema hayo jana baada ya kufanya mazungumzo na Lowassa, ambaye ni mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema kupata taarifa ya kikao chake na Rais kilichofanyika Jumanne iliyopita Ikulu, Dar es Salaam.
Tangu Ikulu itoe taarifa ya mazungumzo ya Lowassa na Rais, viongozi wa Chadema wamepokea suala hilo kwa hisia tofauti, wengi wakimkosoa mbunge huyo wa zamani wa Monduli kwa kusifia juhudi za Rais Magufuli bila ya kueleza kasoro za Serikali ya Awamu ya Tano katika kushughulikia demokrasia, uhuru wa habari, mikutano ya hadhara na masaibu wanayokabiliana nayo viongozi wa upinzani dhidi ya vyombo vya dola.
Aboubakary Liongo, ambaye ni msemaji wa Lowassa, alieleza jana kwamba waziri huyo mkuu wa zamani alifanya mazungumzo na Mbowe kwa lengo la kumpa mrejesho ya kile kilichojiri Ikulu.
Baada ya taarifa hiyo ya Liongo, Mwananchi iliwasiliana na Mbowe ambaye alithibitisha kuwapo kwa mazungumzo hayo na Lowassa.
“Ni kweli nilikutana na Mheshimiwa Lowassa na tulizungumza, lakini siwezi kutoa kila kitu. Tulichozungumza si kwa public (watu wote), lakini muda ukifika kama itahitajika tutafanya hivyo,” alisema Mbowe.
“Ieleweke kwamba, Ikulu walitoa taarifa ya dakika tano waliyoona wao inafaa. Kama wanataka watoe mazungumzo yote ya zaidi ya saa moja na nusu waliyofanya, si kuchagua kipi kiende na kipi kisiende kwa masilahi yao.
“Kama Ikulu inataka iweke full text (taarifa yote) ya mazungumzo, si kutoa vitu nusunusu kwa masilahi yao. Kama wanataka kumchonganisha (Lowassa) na wenzie wameshindwa.”
Hata hivyo, Mbowe hakueleza kama alikuwa na taarifa za kikao cha Lowassa na Rais baada ya kuulizwa na Mwananchi, badala yake alijibu swali jingine la kipi kitarajiwe. “Kama nilivyosema mwanzo, mazungumzo yalikuwa ya faragha, sidhani kama mazungumzo ya faragha unaweza kuyaweka wazi, ila muda ukifika ikihitajika tutafanya hivyo.
Tamko la Mbowe ambaye pia ni Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, baada ya kukutana na Lowassa linaweza kutuliza joto ambalo lilikuwa linaonekana kuanza kupanda kutokana na kila mmoja kutoa kauli yake dhidi ya waziri huyo mkuu wa zamani.
Miongoni mwa waliotoa kauli hizo ni Mbowe mwenyewe juzi, ambaye alisema sifa alizotoa Lowassa ni maoni yake binafsi na si msimamo wa Chadema, huku akisema mtu anayemsifu Magufuli anahitaji “ujasiri wa ziada”.
Mwingine ni Mwanasheria Mkuu wa Chadema, Tundu Lissu ambaye alihoji sababu za Lowassa kutomtaarifu Mbowe kuhusu mwaliko wake Ikulu wakati walikutana siku chache zilizopita.
Pia mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema alihoji sababu za Lowassa kummwagia sifa Rais wakati hali ya kiuchumi ikiwa mbaya kutokana na biashara kufungwa; wapinzani wakikamatwa kila mara; mikutano ya hadhara ikiwa imepigwa marufuku; vyombo vya habari kufungiwa; watu kupotea na Lissu kushambuliwa kwa risasi.
Hata Umoja wa Vijana wa Chadema (Bavicha) ulimlaumu Lowassa kwa kupongeza bila ya kuzingatia masuala mengine yanayoendelea nchini.
Kauli hizo zilionekana kuanza kupandisha joto Chadema kabla ya Mbowe kukutana na mgombea huyo wa urais mwaka 2015 kupitia Chadema akiungwa mkono na vyama vinavyounda Ukawa na kuzungumza.