Nyumba ya kiongozi wa upinzani yapigwa bomu

Makamu wa Rais wa zamani wa Kenya ambaye sasa ni kiongozi mwenza wa NASA, Stephen Kalonzo Musyoka nyumba yake imepigwa bomu usiku wa kuamkia leo katika eneo la Karen, Nairobi Kenya na watu wasiojulikana.

Maafisa wa polisi nchini Kenya wamezingira makazi ya kiongozi huyo leo mapema baada ya usiku watu wasiojulikana kurusha bomu la mkono na kufyatua risasi katika nyumba hiyo.

Hata hivyo taarifa kutoka nchini Kenya zinasema hakuna mtu aliyejeruhiwa wala kupoteza maisha na polisi wamesema watatoa taarifa kamili baada ya kukamilisha uchunguzi wao kufuatia tukio hilo.

Kalonzo Musyoka jana Januari 30, 2018 alishindwa kutokea kwenye sherehe za kujiapisha kwa kiongozi Mkuu wa upinzani nchini Kenya Bwana Raila Odinga kuwa Rais wa wananchi wa Kenya sherehe zilizofanyika bustani ya Uhuru jijini Nairobi.