Serikali imesema hakuna vikwazo katika uhamisho wa walimu na kutaka jambo hilo lifanywe na wahusika kwa kufuata taratibu.
Kauli hiyo imetolewa leo Januari 30, 2018 bungeni mjini Dodoma na Naibu Waziri Ofisi ya Rais (Tamisemi), Joseph Kakunda wakati akijibu swali la msingi la mbunge wa Viti Maalumu (CUF), Rehema Juma Migilli.
Migili alitaka kujua ni lini Serikali itaondoa vikwazo kandamizi kwa walimu wanaotaka kuhama vituo vyao vya kazi kwa hiyari kutokana na
sababu mbalimbali.
Pia, amehoji lini Serikali itatoa mafunzo kwa walimu wanaotolewa shule za sekondari na kupelekwa shule za msingi ili waweze kuendana na mitaala inayofundishwa huko.
Katika majibu yake, Kakunda amesema walimu wanaozingatia taratibu zote na kanuni za utumishi huweza kuhamishwa bila shida.
“Mfano, katika kipindi cha Julai 2017 hadi Januari 2018, walimu 2,755 kwa nchi nzima walihamishwa na wengine taratibu zinaendelea,” amesema.
Kuhusu kuwapa mafunzo walimu wanaohamishwa kutoka sekondari kwenda msingi, amesema hawawezi kupewa mafunzo kwa sababu wengi walipandishwa kutoka msingi kwenda sekondari.
Kuhusu malipo ya uhamisho kwa walimu hao, amesema hawawezi kulipwa kwa sababu wengi wao hawapelekwi mbali na maeneo yao ya kazi ya awali.