BAADA ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) hivi karibuni kumtangaza mshambuliaji wa Simba, John Bocco kuwa mchezaji bora wa mwezi Januari, mwenyewe amesema kuwa kazi ndiyo kwanza imeanza.
TFF ilimtangaza Bocco kuwa mchezaji bora wa mwezi Januari baada ya kumbwaga mchezaji mwenzake wa Simba, Mganda Emmanuel Okwi pamoja na Kiungo wa Mwadui FC, Awesu Awesu.
Akizungumza na Championi Jumatano kuhusiana na tuzo hiyo, Bocco alisema kuwa anashukuru kwa kuipata lakini pia imemfanya aongeze bidii ili kuhakikisha anaisaidia Simba kutwaa ubingwa wa ligi kuu msimu huu.
Alisema kuanzia sasa atahakikisha anapambana vilivyo uwanjani kila atakapopewa nafasi ya kuitumikia Simba na atafanya hivyo bila ya kujalisha timu atakayokutana nayo.
“Nimefurahi kupata tuzo hiyo na imeniongezea nguvu ya kuhakikisha napambana vilivyo uwanjani ili kuisaidia timu yangu kupata matokeo mazuri.
“Kwa hiyo kazi ndiyo kwanza imeanza, nitapambana kwelikweli na hata kama ni kufia uwanjani basi iwe hivyo,” alisema Bocco ambaye amejiunga na Simba msimu huu akitokea Azam FC na baada ya muda mchache akachaguliwa kuwa nahodha wa timu hiyo.