Dereva na kondakta wa daladala alilopanda mwanafunzi wa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT), Akwilina Akwiline aliyeuawa juzi kwa kupigwa risasi na polisi wamesimulia mkasa ulivyokuwa.
Akwilina alikuwa mwanafunzi wa mwaka wa kwanza wa Shahada ya Ununuzi na Ugavi (Procurement and Logistics) katika chuo hicho, lakini maisha yake yalikatishwa juzi akiwa ndani ya basi la daladala.
Tukio hilo lilitokea wakati polisi wakiwatawanya wanachama wa Chadema wakiongozwa na mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe waliokuwa wakielekea katika ofisi ya msimamizi wa uchaguzi Jimbo la Kinondoni, Aaron Kagurumjuli kudai hati za viapo vya mawakala wao.
Jana, Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa alikiri kuwapo kwa kifo cha mtu mmoja aliyepigwa risasi na askari wakati wakizuia maandamano hayo. Wakizungumza na Mwananchi, kondakta na dereva wa daladala alilokuwa amepanda mwanafunzi huyo akitokea katika chuo hicho eneo la Mabibo kwenda Makumbusho walisema alipigwa risasi wakiwa Mkwajuni, Kinondoni baada ya kuwakuta wafuasi wa Chadema wakiandamana.
Kondakta Abbas Abdallah ambaye katika tukio hilo alijeruhiwa kwa risasi kichwani, alisema mwanafunzi huyo alipanda basi hilo kwenye kituo cha NIT Mabibo saa kumi na moja jioni. Alisema alipokuwa akiingia kwenye gari mwanafunzi huyo alikuwa akiongea kwa simu na hakukaa kwa sababu hakukuwa na kiti kilichokuwa wazi.
“Daladala iliendelea na safari kama kawaida, tulipakia na kushusha abiria. Tulipofika kituo cha Magomeni Kanisani abiria walikuwa wamepungua, hivyo yule dada alikwenda kukaa siti ya mwisho kabisa,” alisema.Alisimulia kuwa wakiwa kwenye mteremko wa Mkwajuni, aliona kundi la watu mbele yao huku kukiwa na magari ya askari lakini wao waliendelea na safari.
“Wakati huo nilikuwa nimetoka nyuma kuchukua nauli, ile narudi kwenye mlango nikashangaa kelele za abiria ile nageuka nijue kuna nini nikaona kitu kimepita sikioni shaa! kumbe ilikuwa risasi.
“Kabla sijafanya chochote wakati huo nashangaa dereva akaniambia lala chini umeshaumia, ile nainama nikashangaa damu inamwagika kumbe risasi ilikuwa imenipitia.” Dereva wa daladala hilo, Shaaban Mohammed alisema aliposikia milio ya risasi huku ndani ya basi abiria wakipiga kelele, aliamua kusimama ili ajue kinachoendelea. Alisema kwa sababu nje kulikuwa na fujo, huku ndani ya basi abiria mmoja akiwa ameanguka, ilibidi awaamrishe abiria wote walale chini kuokoa uhai wao kwa kuwa alishaona risasi zinapigwa.
“Kondakta wangu naye damu zilikuwa zinamwagika nikamwambia alale haraka, kwa hiyo wote tulikuwa tumechanganyikiwa wakati huo,” alisema Mohammed.
Alisema wakati hayo yakitokea ilikuwa takriban saa 11:30 jioni.
“Gari lilitapakaa damu na mwanafunzi aliyekuwa amepigwa risasi alikuwa ameanguka, kila mtu akawa haelewi nini kifanyike,” alisema. Baada ya tukio hilo, dereva huyo aliamua kuondoa basi katika eneo hilo na alipofika Kinondoni Studio alimuona askari wa usalama barabarani (trafiki) na kumweleza kilichotokea akimuomba msaada na hiyo ikiwa ni baada ya kubaini kuwa mwanafunzi huyo alikuwa ameshafariki dunia.
Alisema alielekezwa kwenda kituo kidogo cha polisi kilicho jirani na ukumbi wa Vijana CCM Kinondoni na baada ya kufika na kujieleza, hawakuandikisha maelezo yoyote wala kupewa karatasi, bali waliongozana na askari aliyekuwa amevalia kiraia hadi Hospitali ya Mwananyamala.
“Mwili wa yule mwanafunzi ulishushwa,” alisema Mohammed ambaye alieleza kuwa ni mgeni jijini Dar es Salaam alikofika mwezi uliopita akitokea Tanga.
Kondakta Abdallah alisema alipatiwa huduma ya kwanza na aliandikiwa dawa ambazo bado hajanunua kwa kukosa fedha.
“Najihisi kichwa kizito, kinauma na niliandikiwa dawa, hivyo namsubiri bosi wangu nipate fedha za matibabu,” alisema.
Dereva Mohammed alisema tangu tukio hilo la juzi lililosababisha vioo vya gari kuvunjika wameliegesha basi hilo wakiamini watafidiwa kwa uharibifu huo ili waendelee na kazi za kila siku.
Shuhuda mwingine
Shuhuda mwingine wa tukio hilo, Noel Shao ambaye alikuwapo wakati mwili wa marehemu ukifikishwa Mwananyamala alisema, “Nilishiriki katika kuuhifadhi mwili wa Akwilina. Alivalia suruali ya jeans iliyokuwa na takriban Sh25,300 tena noti za elfu tano tano, ambazo alikabidhiwa ndugu yake baada ya kufika. Hakika lilikuwa ni tukio la kusikitisha sana.”
Simulizi chuoni NIT
Baada ya taarifa za kifo cha mwanafunzi huyo kufika NIT, vilio, huzuni na majonzi vilitawala. Hata jana mchana wakati waandishi wetu walipofika chuoni hapo, waliwakuta wanafunzi wakiwa katika vikundi huku karibu wote wakiwa na nyuso za huzuni.
Hata hivyo, licha ya kusema kwamba wamepata taarifa za tukio hilo uongozi wa NIT kupitia kwa Ofisa Uhusiano, Ngasekela David ulisema suala hilo lipo katika mikono ya polisi na familia yake.
“Tulipata taarifa za msiba wa mwanafunzi huyu kutoka kwa mwanafunzi mwenzake aliyekuwa anaishi naye nje ya chuo, tumesikitishwa na kifo chake hivyo tunaendelea kuwasiliana na familia kujua utaratibu,” alisema. Rafiki wa mwanafunzi huyo, Hidaya Shaaban alisema Akwilina alimuaga kuwa anaelekea Bagamoyo mkoani Pwani kupeleka barua ya mafunzo kwa vitendo.
“Najisikia vibaya na nimeumia, aliniaga anaenda kupeleka barua yake ya ‘field’ na alikuwa nayo kweli, jioni nikashangaa kupata taarifa kuwa amepata ajali na sikujua ajali gani lakini baadaye nikaambiwa mauti imemfika,” alisema.
Alisema awali hakujua kama alifariki dunia kwa kupigwa risasi.
Paul Sabuni ambaye ni kiongozi wa darasa alilokuwa akisoma Akwilina, alisema kabla ya kifo chake alifika chuoni kusaini ‘course work’.
“Alikuja saa tisa kuangalia matokeo yake na kwa kweli alikuwa amefanya vizuri, alikuwa msichana mzuri anayejituma darasani, tumeumia mno. Sikuwahi kusikia kama anajihusisha kwa namna yoyote na siasa wala chama,” alisema Sabuni ambaye ni waziri wa mikopo wa serikali ya wanafunzi wa NIT.
Ndugu wa wamlilia
Tugolena Richard Uiso, ambaye ni dada wa Akwilina akizungumza na Mwananchi alisema familia ilishtushwa na taarifa za kifo chake.
Alisema awali hawakuamini kwa sababu walijua yupo chuoni.
“Jana jioni (juzi) tulipata taarifa amepigwa risasi Kinondoni na amepelekwa hospitalini Mwananyamala, tulishangaa ikabidi twende kuhakikisha ile taarifa,” alisema.
Alisema baada ya kwenda hospitalini waliutambua mwili na kuthibitisha kuwa ndiye mtoto wao.
“Leo asubuhi wenzetu wameamkia Polisi Oysterbay, wameambiwa mwili utapelekwa Muhimbili kwa ajili ya uchunguzi zaidi, tumebaki na simanzi tunasubiri kinachoendelea,” alisema.
Alisema Akwilina ni mtoto wa sita kwa wazazi wake wanaoishi Olele wilayani Rombo mkoani Kilimanjaro wakijishughulisha na kazi za kilimo na ufugaji na alifika Dar es Salaam kwa ajili ya masomo.
Kauli za wadau
Kutokana na tukio hilo, Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu katika taarifa kwa vyombo vya habari umesema umepokea kwa masikitiko kifo cha mwanafunzi huyo.
“Mauaji haya ya kikatili yanasikitisha sana na sisi kama watetezi wa haki za binadamu tunalaani vikali vitendo hivyo kwa kuwa ni kinyume kabisa na haki za binadamu,” inasema taarifa hiyo iliyosainiwa na mratibu wake Onesmo Olengurumwa.
“Tunaviomba vyombo husika kuchukua hatua stahiki kwa waliotekeleza mauaji ya raia wasiokuwa na hatia,” alisema.
Chama cha ACT Wazalendo kimesema kimepokea kwa masikitiko tukio la mauaji ya mwanafunzi huyo.
“Tunasikitika na tunakataa kuona Tanzania inaingia katika ubaguzi wa vyama. Utu na heshima ya binadamu wa Tanzania hauwezi kupimwa na uvyama,” inasema taarifa hiyo iliyotolewa na mwenyekiti wake, Yeremia Maganja akiwaomba viongozi wa dini na makundi mengine ya jamii kukemea mauaji hayo.