F Mkurugenzi wa ICC kufanya mazungumzo na Waziri Kabudi | Muungwana BLOG
https://c2p.cleverwebserver.com/dashboard/6a0bec4b-79ba-11ef-ad2b-06f0639468d1

Mkurugenzi wa ICC kufanya mazungumzo na Waziri Kabudi


MKURUGENZI wa Masuala ya Ushirikiano wa Mahakama ya Kimataifa ya Makosa ya Jinai (ICC), Phakiso Mochochoko, ametua nchini na ujumbe wake na kufanya mazungumzo na Waziri wa Katiba na Sheria, Prof. Palamagamba Kabudi.

Mazungumzo hayo yalifanyika juzi jijini Dar es Salaam katika Ofisi Ndogo ya Wizara hiyo.

Mochochoko yuko ziarani nchini kukutana na viongozi wa serikali kuelezea mipango na utendaji wa mahakama hiyo katika Bara la Afrika.

Katika mazungumzo yao, Mochochoko alimweleza Prof. Kabudi kuwa ICC inaridhishwa na ushirikiano ambao imekuwa ikipatiwa na Tanzania.

Alimhakikishia Prof. Kabudi kuwa mahakama hiyo inathamini mchango wa Tanzania katika kuhakikisha inatekeleza majukumu yake.

Kwa pande wake Prof. Kabudi alimhakikishia Mochochoko kwamba Tanzania ikiwa  mwanachama wa ICC, itaendelea kuunga mkono jitihada za ICC katika kuhakikisha amani na utulivu vinatamalaki katika Bara la Afrika na duniani kote na kwamba vitendo vyote vya kijinai vinachukuliwa hatua kwa mujibu wa Mkataba wa Rome.

Prof. Kabudi alisema upatikanaji wa amani katika nchi za Afrika, zikiwamo nchi jirani na Tanzania, unaisaidia Tanzania katika kujiletea maendeleo yake.

Alisema kuwapo kwa amani na utulivu kutasaidia kupunguza muda wa kuzisaida nchini hizo hasa kwa kuhifadhi raia wa nchi hizo ambao watakimbilia nchini na kuwa wakimbizi.