F Naibu Spika aweka wazi siri ya utulivu bungeni | Muungwana BLOG
https://c2p.cleverwebserver.com/dashboard/6a0bec4b-79ba-11ef-ad2b-06f0639468d1

Naibu Spika aweka wazi siri ya utulivu bungeni


Tulia afichua siri  utulivu bungeni

NAIBU Spika wa Bunge, Dk. Tulia Ackson, amesema siri kubwa ya wabunge kutosusia vikao vya Bunge katika kipindi hiki ni wabunge kuelewa kanuni na kuzifuata.

Tulia aliyasema hayo jana wakati akihojiwa kituo cha redio cha  East Africa na kueleza kuwa, wabunge kwa sasa wameelewa utaratibu wa namna ya uendeshaji wa vikao vya Bunge kwa sasa wanasikiliza maelekezo wanayopewa.

“Badala ya kubishana na yule anayewaelekeza, wanamsikiliza kwa kadri wanavyoongozwa kikanuni na kufuata maelekezo wanayopewa, hii ndiyo siri kubwa,” alisema Dk. Tulia.

Aidha, alisema hali hiyo imesababisha vikao vya Bunge vya sasa kutokuwa na mivutano.

Alisema kwa sasa mbunge akiambiwa akae anakaa na hiyo haitekelezwi kwake tu bali hata kwa Mwenyekiti akiongoza vikao vya Bunge.

“Wameelewa utaratibu wa namna ya uwendeshaji vikao vya Bunge, wanasikiliza maelekezo wanayopewa akiambiwa akae anakaa, sio kwangu tu hata kwa Mwenyekiti anapoongoza vikao, mwanzoni kulikuwa na changamoto hizo mtu haelewi kwa nini mtu mwingine amzue kuzungumza,” alisema.

Katika mahojiano hayo, Dk.Tulia alizungumzia pia kuhusu mbio zinazojulikana kama ‘Mbeya Tulia Marathon 2018’ zinazotarajia kufanyika Mei 6.

Alisema mashindano hayo yatafanyika katika viwanja vya Sokoine mkoani Mbeya na washiriki wa mbio za kilomita 42 ni Sh. 30,000, kilomita 21 ada ni Sh. 20,000, mbio za baiskeli Sh. 20,000 na wengine watalipa Sh. 10,000.

Alisema fedha zitakazokusanywa ni kwa ajili ya kujenga mabweni ya kike kwa sababu lengo ni ili wasome katika mazingira mazuri.

“Wakati nasoma, mazingira yangu ya shuleni siyo kwamba yalikuwa mazuri sana au rahisi, nilisoma katika mabweni, lakini tulikuwa wanafunzi wachache wakati huo, sasa hivi wanafunzi ni wengi,” alisema.

Aliongeza: “Shule za kata zilizojengwa zimesababisha kuwapo kwa wanafunzi wengi wanakwenda sekondari na wengi wanatoka majumbani, shule za kata zina madarasa na nyumba za walimu, lakini hazina mabweni ndiyo maana tumeona tuanze kujenga mabweni,” alisema.

Wanatarajia kuchangisha Sh. 300,000,000 kwa ajili ya kujenga mabweni ya watoto wa kike kwenye shule za sekondari za kata.

Akizungumzia fao la kujitoa, Dk. Tulia alisema kwa sasa halipo, badala yake limeletwa Fao la Kukosa Kazi, ambalo litamwezesha mtu kupewa mafao yake kwa kipindi ambacho kinakubalika kimataifa.

“Fao la Kukosa Kazi halimaanishi mtu atapewa mafao yake yote hapana, bali kwa kipindi cha miezi sita ambacho tunaamini asiye na kazi atatafuta na kupata, hivyo wakati akitafuta kazi mfuko wa jamii utampa fao la kukosa kazi,” alisema.

Katika hatua nyingine, Dk. Tulia alisema hoja binafsi ya Mbunge wa Viti Maalum (Chadema), Upendo Peneza, ya kuiomba Serikali kutoa bure kwa wanafunzi taulo za kujihifadhi wanawake wakati wa hedhi ni nzuri na kushauri ili iweze kupitishwa, anatakiwa kuzungumza na wabunge wengi ili ikipelekwa bungeni ipite.

“Hoja hii ni nzuri, ila kwa sababu bado haijaletwa bungeni, ni vizuri mbunge husika akazungumza na wabunge wengi ili waikubali ili ikifika bungeni ipite,” alisema.