Dar es Salaam. Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imejikuta matatani baada ya wadau, maofisa wa benki na viongozi wa dini kuhoji uhalali wa mamlaka hiyo kuweka hadharani taarifa za fedha za Kanisa la Full Gospel Bible Fellowship (FGBF).
Juzi, TRA ilitoa taarifa ya uchunguzi ilioufanya kuhusu kauli ya kiongozi wa kanisa hilo Askofu Zachary Kakobe aliyoitoa wakati wa ibada ya mkesha wa Krismasi mwishoni mwa mwaka jana kuwa ana fedha nyingi kuliko Serikali.
Kamishna Mkuu wa TRA, Charles Kichere alisema wangefanya uchunguzi kuhusu kauli hiyo, lakini taarifa aliyoitoa juzi ilionyesha kuwa Askofu Kakobe hana akaunti katika benki yoyote nchini bali ni mmoja wa wasimamizi wakuu wa akaunti ya kanisa analoliongoza.
Kichere alisema akaunti za kanisa hilo zipo katika benki ya NBC zikiwa na zaidi ya Sh8 bilioni na zinatokana na fedha za sadaka, zaka na changizo zinazotolewa na waumini.
Kichere alipotafutwa na Mwananchi jana kuhusu hatua ya kutangaza taarifa za kifedha za kanisa hilo alisema taarifa yake kwa vyombo vya habari inaeleweka na inajieleza hivyo hawezi kutoa maoni zaidi.
“Wakati nataka kufanya uchunguzi nilieleza wazi nia yangu, hata baada ya kumaliza uchunguzi niliona ni busara kusema yaliyobainishwa katika uchunguzi, sitaki ‘ku-comment’ (kutoa maoni) zaidi, mjadala wa masuala ya Kakobe ulishafungwa,” alisema Kichere.
Akizungumzia taarifa ya TRA, ofisa mwandamizi wa benki moja nchini ambaye hakutaka utambulisho wake uwekwe hadharani alisema kitendo cha mamlaka hiyo kutoa taarifa za fedha kwa umma ni uvunjifu wa sheria.
Alisema kwa mujibu wa sheria taarifa za kibenki zinapokuwa zinahitajika na vyombo au mamlaka za Serikali zinaweza zikatolewa mahakamani, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa au polisi lakini si kwa umma.
Alisema Askofu Kakobe ana nafasi kubwa ya kuwafungulia mashtaka uongozi wa benki na mamlaka iliyotoa taarifa zake kwa umma.
Mkurugenzi mtendaji wa benki (jina limehifadhiwa) alipoulizwa kuhusu utaratibu wa kawaida wa utunzaji wa siri za mteja alisema sheria ya huduma za benki inaelekeza vizuri kuhusu jambo hilo lakini taarifa zinaweza kutolewa kwa mujibu wa sheria kutokana na mazingira na madhumuni fulani.
Alisema hata pale ambapo taarifa zinaonekana ni muhimu kutolewa kwa mamlaka yoyote ya Serikali iliyokidhi vigezo, bado hairuhusiwi kuziweka kwa wazi bali inapaswa kuzitumia kwa kazi yake tu kwa kuwa kuzichapisha kwa namna yoyote ni kuvunja sheria.
“Suala la taarifa za mteja ni siri kubwa ndiyo maana hata ofisa wa benki hana namba ya siri ya mteja. Inapotokea taarifa za mteja zimetolewa halafu zikachapishwa na ile mamlaka iliyopewa taarifa hizo, mteja anaweza akafungua kesi ambayo ni kubwa dhidi ya benki na hiyo mamlaka,” alisema.
Suala hilo halikuwapita viongozi wa dini, kwani nao walikuwa na maoni yao.
Askofu Benson Bagonza wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Karagwe alisema hatua hiyo ni mbaya na haikubaliki kwa taasisi za dini.
“Hiyo ni mbaya sana. Kama Askofu Kakobe asingesema kile alichosema asingechunguzwa. Kwa hiyo kama hutaki kuchunguzwa usiseme kitu? Kwa hiyo maisha yetu yanakwenda mbali hadi kwenye mali za kanisa?” alihoji Askofu Bagonza.
Kauli hiyo iliungwa mkono na Mwenyekiti wa Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT), Dk Alinikisa Cheyo aliyeitaka TRA kufuata maadili ya kazi.
“Nafikiri TRA wana maadili wanaposhughulika na wateja wao. Huwezi kuweka wazi madeni na mali za mteja wako. Si makanisa tu hata wateja wa kawaida, labda ni kwa sababu ya mlolongo wa yaliyotokea.” alisema Dk Cheyo.