Zanzibar/Dar. Wiki mbili baada ya Serikali kuzindua utoaji wa hati za kusafiria za kielektroniki, baadhi ya wajumbe wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar wameitaka mamlaka husika kuifanyia marekebisho pasipoti hiyo.
Marekebisho ambayo wawakilishi hao wanayataka katika pasipoti hiyo kuwa na mwonekano wa Muungano.
Wajumbe hao walisema hayo jana walipokuwa wakichangia ripoti ya kamati ya kusimamia ofisi za viongozi wakuu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kikao cha Baraza la Wawakilishi kinachoendelea, Chukwani nje kidogo ya mji wa Zanzibar.
Walisema kwa kuwa suala la hati ya kusafiria ni la Muungano, ilipaswa mwonekano wa hati hiyo mpya kubeba pande zote mbili; Zanzibar na Tanzania Bara.
Mwakilishi wa Chaani, Nadir Abdul-latif Jussa alisema anashangazwa kuona ndani ya hati hiyo kuonekana picha ya Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere pekee huku ya Baba wa Taifa la Zanzibar, hayati Abeid Amani Karume ikikosekana.
Alisema hilo halileti taswira nzuri kwa upande wa wananchi wa Zanzibar kutokana na viongozi hao wawili kuwa waasisi wa Muungano.
“Cha kushangaza zaidi hata huko kwenye mfumo wa kujaza kwa njia ya kielektroniki hakuna tena neno Zanzibar kama sehemu iliyotolewa hati hiyo, badala yake sasa unajaziwa sehemu unakotokea tu kwa mfano, Mkoa wa Kusini, Kaskazini au Mjini bila ya kuonyesha Mjini wapi,” alisema Jussa.
Alisema, “Kitendo cha kutokuwepo kwa neno Zanzibar kama ni sehemu ya mtu anayotoa kama ilivyo katika pasipoti za zamani ni kuidharau kabisa Zanzibar.”
Jussa alisema kwa kuwa waliopewa pasipoti hizo hawafiki hata watu 100, ni vyema wahusika wakuu wa suala hilo kufanya haraka kubadili mwonekano na muundo wake ili kutoa usawa kwa pande zote za Muungano.
Mwakilishi wa Shaurimoyo, Hamza Hassan Juma alisema suala la hati za kusafiria linahitaji kutazamwa kwa kina zaidi kwa pande zote mbili za Muungano ili kuwepo kwa haki sawa.
Akitoa mfano, alisema yeye ni miongoni mwa waliojaza fomu za kupatiwa pasipoti mpya lakini neno Zanzibar hakuliona hivyo kupata wasiwasi... “Hivyo kuna haja ya hati hiyo kuboreshwa.”
Wakati wajumbe hao wakilalamikia hati hizo, Idara ya Uhamiaji imewatahadharisha wananchi kuwa makini na waliokuwa watumishi wake walioacha kazi kwa sababu mbalimbali ikiwamo kufukuzwa mwaka 2016/17. Kamishna Jenerali wa Uhamiaji, Dk Anna Makakala alisema jana kuwa kati ya watumishi hao 18, baadhi yao wamekuwa wakiendelea kujinasibisha kama bado ni wa idara hiyo.
Alisema idara imewatangaza hadharani ili kuisaidia jamii kuwatambua kwamba si watumishi wa Uhamiaji, hivyo ikitokea miongoni mwao akaendelea kujitambulisha, wachukue hatua ikiwamo kuwafikisha katika vyombo vya sheria.
Aliwataka watumishi hao kuwa ni Thobias Lyewe, Julieth Mrema, Nina Mliga, Loveness Wilson, Wilbard Ompapson, Salama Dilunga, Philbert Chaula, Mkombozi Chodri na Alfred Mrema.
Wengine ni Imakulata Mwakatika, Ramadhani Ally, Ritha Maganga, Jovin Mkuchu, Veronika Max, Angela Mwambwiga, Peter Bally, Elizabeth Kibinga, na Lucy Munyanga. Msemaji wa Uhamiaji, Ally Mtanda alisema, “Kuna shida inatokea kwa watu wengi kujitambulisha kuwa wanatoka Uhamiaji. Wanakwenda viwandani na maeneo mengine kisha kuwarubuni watu na kuchukua fedha.
“Wale kwa namna moja au nyingine walifukuzwa kazi na wengine wameacha wenyewe lakini wanaendelea kujitambulisha kuwa watumishi ndiyo maana tumeamua kutoa orodha ili wananchi wawatambue kwamba hawa si watumishi wetu na hatutahusika kwa lolote likitokea,” alisema.