F Amuua mkewe kisha naye kujinyonga | Muungwana BLOG
https://c2p.cleverwebserver.com/dashboard/6a0bec4b-79ba-11ef-ad2b-06f0639468d1

Amuua mkewe kisha naye kujinyonga

Mwanaume mmoja anatuhumiwa kumuua mkewe kwa kumchoma na kitu chenye ncha kali sehemu za mwili wake kisha na yeye mwenyewe kujinyonga hadi kufa kwa kutumia waya wa umeme wilayani Magu ambapo kitendo hicho ni kosa kisheria.

Akithibitisha kutokea kwa tukio hilo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza Naibu Kamishna wa Polisi, Ahmed Msangi amesema kuwa mtu huyo ametambulika kwa jina la John Ntemi (23) mkazi wa Kijiji cha Mahaha ambaye anatuhumiwa kumuua mkewe Casta Edward.

Aidha, Kamanda Msangi amesema inadaiwa wawili hao walikuwa wanaishi peke yao na kabla ya tukio hilo kutokea wanandoa hao walikuwa wakiishi kwa amani na upendo bila ya mgogoro wa aina yeyote kati yao, lakini ilipofikia Machi 26, 2018 majira ya saa 6:00 mchana mwenye nyumba waliyopanga alipita karibu na maeneo ya nyumba yao ndipo alipoona damu chini ya mlango, na kuweza kutoa taarifa kwa majirani pamoja na Jeshi la Polisi.

Pamoja na hayo, Kamanda Msangi amesema polisi walipofika katika eneo la tukio waliweza kukuta mwili wa mwanamke ukiwa mlangoni ndani ya nyumba eneo la tukio likionesha miburuzo ya damu toka chumbani hadi mlangoni huku mlango ukiwa umefungwa kwa kufuli.

Uchunguzi wa awali unaonesha mauji hayo yalitekelezwa usiku wa Machi 25, 2018 kutokana na kuwepo kwa mvua kubwa katika kijiji hicho kiasi kwamba majirani wasingeweza kusikia kilichokuwa kikiendelea ndani kwa wawili hao.