F BASATA yakanusha kuzifungulia nyimbo mbili za Diamond | Muungwana BLOG
https://c2p.cleverwebserver.com/dashboard/6a0bec4b-79ba-11ef-ad2b-06f0639468d1

BASATA yakanusha kuzifungulia nyimbo mbili za Diamond

Staa wa muziki wa Bongo fleva Diamond Platnumz.

Baraza la Sanaa la Taifa (Basata), limesema nyimbo mbili za Diamond, hazijafunguliwa kama inavyodhaniwa.

Katibu Mtendaji wa Baraza hilo Godfrey Mngereza amesema nyimbo za Wakawaka na Hallelujah hazijafunguliwa na jambo hilo halina ukweli wowote na kuwataka wananchi kulipuuza.

 Kadhalika, Mngereza ametoa ufafanuzi kwa nini msanii Diamond amekutana na Waziri wa Habari, Utamaduni,Sanaa na Michezo, Dk Harrison Mwakyembe na Naibu wake, Juliana Shonza na sio wasanii wengine.

 Mngereza ametoa ufafanuzi huo baada ya kusambaa kwa taarifa iliyoeleza msanii huyo kakutana na mawaziri hao.

Baada ya taarifa hizo, kulizuka gumzo mitandaoni ambapo watu walihoji kwa nini wakutane na msanii huyo wakati kuna waliofungiwa nyimbo zao kama yeye na wengine kufungiwa kufanya muziki kwa miezi sita.

 Mngereza amesema hatua hiyo imetokana na majibizano yaliyokuwa yanaendelea kati ya Diamond na naibu waziri Shonza na ndio sababu iliyowafanya wawili hao wakutanishwe meza moja ili kuyamaliza.

Akihojiwa katika kituo cha Redio Times FM, Diamond alisikika akimrushia maneno moja kwa moja Shonza kuwa amekuwa akiwafungia wasanii nyimbo zao na kuwafungia wasifanye kazi kwa lengo la kutafuta umaarufu na kuogopa kutumbuliwa.

 Hata hivyo, kwa upande wake Shonza alisema hayupo tayari kujibizana na msanii huyo mitandaoni kwa kuwa aliyemfungia si yeye, bali ni serikali na kumtaka kufuata taratibu kama anaona ameonewa ikiwemo kufika Basata, Wizarani au kuandika barua, jambo ambalo Diamond alilitekeleza siku ya Ijumaa.

Akizungumzia hilo, Mngereza alitaka wananchi waelewe kwamba malumbano hayo ndicho chanzo cha Diamond kukutana na mawaziri hao na kuwataka kuondoa dhana kama mtu aliyepewa upendeleo katika sakata la kufungia nyimbo.

Alipoulizwa kuhusu kukutana na wasanii wengine wenye malalamiko amesema mpaka sasa hajapata barua yoyote ya wasanii hao kutaka kuonana nao.