Baada ya Yanga kutolewa kwenye michuano ya ligi ya Mabingwa Afrika, kocha wa timu hiyo George Lwandamina amesema hawatarudia makosa badala yake watajipanga vyema ili waweze kufanya vizuri kwenye kombe la Shirikisho.
Lwandamina amesema hayo leo baada ya kuwasili jijini Dar es salaam wakitokea Gaborone Botswana ambapo ameeleza kuwa nguvu zao zote wanahamishia kwenye Kombe la Shirikisho na wana kiu ya kufanya vizuri.
''Ninaamini vijana wamejifunza mengi baada ya kutolewa nje ya Ligi ya Mabingwa Afrika na Township Rollers kwa kufungwa nyumbani sasa watakuwa makini wasirudie makosa'', amesema.
Yanga SC imetolewa kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika jumamosi iliyopita baada ya sare ya 0-0 na wenyeji, Township Rollers huku wakiwa wameruhusu kufungwa mabao 2-1.