MAKAMU wa Rais Samia Suluhu Hassan amesema kitendo cha Hospitali ya Benjamini Mkapa iliyopo Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom), kufanya upandikizaji figo ni hatua kubwa katika maendeleo ya nchi.
Akizungumza jana mjini hapa, Mama Samia alisema serikali inajivunia hatua hiyo na kwamba inafuatilia kwa karibu afya ya mgonjwa aliyepandikizwa figo wiki iliyopita.
Alibainisha kuwa gharama za upandikizaji figo katika hospitali hiyo, ambazo ni Sh. milioni 22 zinaweza kukusanywa katika ngazi za familia na kuokoa maisha ya mgonjwa.
Alipongeza hatua hiyo na kusema itakomboa wananchi wasiokuwa na uwezo, ambao wanaugua ugonjwa huo na kushindwa kwenda India kupata matibabu.
“Tunajivunia hatua hii na serikali inafuatilia kwa karibu afya ya mgonjwa aliyepandikizwa figo," alisema makamu wa rais. "Gharama katika Hospitali ya Benjamini Mkapa sio kubwa sana, ndugu wanaweza kujichanga changa na wakapata matibabu ya kuokoa maisha.”
Wiki iliyopita, hospitali hiyo kwa kushirikiana na madaktari bingwa kutoka Japan ilifanya upasuaji na upandikizaji wa figo kwa mgonjwa mmoja kwa kutumia saa sita.
Upandikizaji huo ulifanywa kwa mgonjwa huyo baada ya mdogo wake wa kike kumpatia figo moja na wagonjwa wote, imeelezwa, wanaendelea vizuri.
Akizungumzia operesheni hiyo, Makamu Mkuu wa Chuo hicho, Prof. Egid Mubofu alisema upandikizwaji huo umeandika historia na kuleta faraja kwa wakazi wa kanda ya kati, kwa kuanza kutoa huduma hiyo.
Figo zinapandikizwa pia Hospitali ya Taifa Muhimbili jijini Dar es Salaam.
“Na huyu ni mgonjwa wa pili kupandikizwa figo hapa nchini. Magonjwa ya figo yameongezeka sana katika ulimwengu wa sasa ikiwamo Tanzania,” alisema Prof. Mubofu.
Mkuu huyo alisema, matarajio yao ni kupandikiza wagonjwa 12 mpaka 20 kila mwaka.
“Hospitali hii kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Dodoma pamoja na Tokushukai Medical Corporation (Shirika la Afya la Tokushukai) tumefanikiwa kufanya upasuaji na upandikizaji figo, tunashukuru uongozi wa hospitali na madaktari wote kutoka Japan na Tanzania walioshiriki zoezi hili,” alisema Prof. Mubofu.
Alibainisha kuwa katika watu 100, asilimia 10 ya mkusanyiko huo huugua maradhi ya figo duniani, Akizungumzia gharama za matibabu, Prof. Mubofu alisema nchini India na kwingineko duniani ni kubwa mno.
Alisema hatua hiyo imeweza kuokoa gharama za kupeleka wagonjwa nje ya nchi ambapo mgonjwa mmoja nchini India hupandikizwa figo kwa Sh. milioni 77 mpaka 80.
Prof. Mubofu alisema kwa Hospitali ya Benjamini Mkapa mgonjwa anaweza kugharimu kiasi cha Sh. milioni 22, hivyo itakuwa imeokoa kiasi kikubwa cha fedha.
Naye Kaimu Mkurugenzi Mkuu Hospitali ya Benjamini Mkapa, Dk. Alphonce Chandika alishauri Watanzania kujiunga na Mfuko wa Bima ya Afya (NHIF), ili kuweza kupata matibabu hayo ndani ya bima.