Kiongozi wa Muungano wa Upinzani nchini Kenya Nasa, Raila Odinga ameweka wazi walichoongea na Rais Uhuru Kenyatta, walipokutana mapema mwezi huu na kwamba waathirika wa ghasia za uchaguzi za mwaka 2017 watalipwa fidia na serikali.
Odinga amesema kuwa pamoja na fidia kulipwa jambo jingine walilokubaliana na Rais Kenyatta ni kufuta kesi za watu walioshiriki kuapishwa kwake, Januari 30 mwaka huu.
Walipokutana viongozi hao wawili walikubaliana kuzika tofauti zao za kisiasa kwa maslahi ya taifa la Kenya ingawa kumekuwa na shauku kubwa miongoni mwa wanasiasa na wananchi kuhusu masuala zaidi waliyokubaliana.
Rais Uhuru Kenyatta pamoja na Odinga walikutana Ikulu Machi 9 ambapo baada ya mazungumzo yao wote walisema kuwa wamekubaliana kuiganisha Kenya kwani nchi hiyo ni kubwa kuliko wao.