F Real Madrid na Lewandowski mambo yameiva | Muungwana BLOG
https://c2p.cleverwebserver.com/dashboard/6a0bec4b-79ba-11ef-ad2b-06f0639468d1

Real Madrid na Lewandowski mambo yameiva

IMERIPOTIWA Real Madrid imefikia makubaliano ya kumsajili mshambuliaji wa Bayern Munich, Robert Lewandowski msimu ujao.

Kwa mujibu wa gazeti la Mundo Deportivo, mwanasoka huyo wa kimataifa wa Poland amefikia makubaliano ya vipengele binafsi kwa mkataba wa miaka miwili na Madrid baada ya mikutano kadhaa mwezi huu.

Rais wa Madrid, Florentino Perez ameamua kumchukua mshambuliaji huyo wa Bayern huku akisikilizia mpango wa kumsajili Neymar kutoka Paris Saint-Germain.

Real imekuwa ikimtaka Lewandowski kwa muda fulani na imefanikiwa kupambana na Chelsea, PSG na Arsenal kuzungumza kwanza na wawakilishi wa mchezaji huyo na inafahamika mshambuliaji huyo anapenda zaidi kuhamia Bernabeu.

Madrid pia imekuwa na dhamira ya kumsajili mshambuliaji wa Tottenham, Harry Kane, lakini haina matumaini ya kuipata saini ya mchezaji huyo kufuatia Mwenyekiti, Daniel Levy kukataa mazungumzo.

Jambo hilo moja kwa moja limegeuza nia ya Perez na kuhamia kwa Lewandowski, ambaye ana rekodi nzuri na amefunga mabao 32 Bundesliga msimu huu.

Anaaminika kuwa mbadala sahihi wa mshambuliaji Mfaransa, Karim Benzema, ambaye amekuwa na msimu mbaya akifunga mabao saba tu katika mechi 31.

Madrid pia inamtaka winga wa Chelsea, Eden Hazard imhamishie Hispania, kwani Mbelgiji huyo yupo katika miezi 15 ya mwisho ya mkataba wake na bado hajasaini mkataba mpya.

Hazard inafahamika bado anasikilizia kama Chelsea itafuzu kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao ndiyo asaini mkataba mpya, vinginevyo atakuwa tayari kuondoka.

Inategemea na mchezaji atakayesajiliwa na Real Madrid juu ya kufungua njia kwa Gareth Bale, ambaye anatakiwa na klabu kadhaa za Ligi Kuu ya England kuondoka.