Wizara ya Kilimo, Maliasili, Mifugo na Uvuvi, inatarajia kukabidhi mashine mbili kubwa kutoka nchini China kwa wajasiriamali wa Zanzibar ambapo moja itatumika kwa ajili ya kukaushia dagaa Maruhubi na moja kwa ajili ya kukamulia ndimu Chwaka.
Mratibu wa mradi wa miundombinu ya masoko, uongezekaji thamani mazao na huduma za kifedha vijijini (MIVARF) kutoka wizara hiyo, Khalfan Masoud Saleh, akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake Maruhubi, alisema mashine hizo ambazo zinatarajiwa kukabidhiwa kwa wajasiriamali hao zina thamani ya shilingi milioni 84.
Alisema mashine ya kukaushia dagaa ina thamani ya shilingi milioni 40 na mashine ya kukamulia ndimu umegharimu shilingi milioni 44.
Alisema kati ya fedha hizo, wajasiriamali hao wamechangia asilimia 25 ya gharama, huku wizara kupitia mradi huo ikichangia shilingi milioni 75.
Alisema hatua hiyo imekuja baada ya ukosefu wa vitendea kazi kwa ajili ya shughuli hizo hasa kipindi cha mvua.
Aidha alisema wakulima wa zao la ndimu wanaotarajiwa kupewa mashine hizo ni ushirika wa UWAMIJICHWA wa Chwaka ambapo una vikundi 19 na wajasiriamali ambapo mashine ya kukaushia daa itatolewa kwa kikundi cha TUSIYUMBISHANE chenye wanachama 160.
Alisema lengo la mashine hizo ni kusanifu na kuyaongezea thamani mazao ya kilimo ili kupata soko la uhakika na kuongeza tija.