ASKOFU wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Dodoma, Amon Kinyunyu amewataka wananchi kuilinda amani, kuishi kwa upendo na kuachana na vitendo vya chuki.
Kauli hiyo aliitoa wakati wa mahubiri ya ibada ya Ijumaa kuu iliyofanyika katika ushirika wa Ipagala, wilayani hapa.
Kinyunyu alisema watu wote wanapaswa kuilinda amani na kuishi kwa kupendana na kusaidiana katika jamii bila ubaguzi.
“Kristo aliupenda ulimwengu na ndio maana akautoa uhai wake kwa ajili yetu sisi wenye dhambi ili tukombolewe tuwe huru na dhambi hivyo huo ni upendo wa agape aliotupenda,”alisema.
Alisema upendo unatakiwa kuanzia kwenye familia wanazoishi kwa kuwapenda ndugu ,watoto pamoja na wote wanaowazunguka.
Alisema kifo cha Yesu msalabani kilikuwa ni upendo wa kipekee ambao alikubali kufa kwa ajili ya wengine wapate ukombozi.
Aidha, alisema wakati wote watu wanatakiwa kuilinda amani ili kuwa na uhuru wa kuabudu na kufanyakazi za kuzalisha mali.
Hata hivyo, alisema maisha ya Yesu Kristo alipokuwa akihubiri duniani alisisitiza amani kwa watu wote kwa sababu alijua bila amani hakuna mafanikio, Erick Kitali, alisema kipindi hiki ni cha watu kushirikiana ili kuonyesha upendo kwa wengine.
“Nchi yetu tumejaliwa amani tunatakiwa kuilinda ili tuweze kuabudu na kufanya kazi zetu kwa uhuru ,tuilinde kama mboni ya macho yetu”alisema.