Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe amesema hotuba za upinzani katika Bunge la Bajeti hazitakuwepo mpaka watumishi wa sekretarieti ya upinzani watakapopatikana.
Mbowe amesema hayo leo jioni wakati akizungumza na Waandishi wa habari mjini Dodoma ambapo amesema kwamba kambi ya upinzania haina hata mtumishi mmoja na hiyo ni kutokana na kufukuzwa na Katibu wa Bunge baada ya mikataba yao kuisha disemba 2017 hali iliyopelekea wao kukosa hata mtaalamu mmoja wa kuandaa hotuba na kuchambua nayaraka.
Aidha kiongozi huyo amesema licha ya kuona tatizo hilo aliomba kibali kwa Spika cha kuweza kuajiri watumishi lakini alipatiwa kibali cha watu watatu tu.
"Watumishi wa upinzani walifukuzwa na Katibu wa Bunge Januari kutokana na mikataba kumalizika Disemba. Nilipomfuata Katibu wa Bunge kumuuliza kulikoni unawafukuza hawa watumishi kama mbwa, akanijibu anafanya kazi kwa mujibu wa kanuni. Ajira zao watumishi msubiri Spika. Hadi leo kambi haina hata mtumishi mmoja. Hatuna hata mtaalamu mmoja wa kuandaa hotuba na kuchambua nyaraka" amesema.
Ameongeza "Sasa kwa hali hii tunapata wapi taarifa ya kuwasilisha bungeni? Watumishi wa CCM hapa bungeni wapo na hawajafukuzwa kama wa kwetu. Alitegemea mimi niandae hotuba Segerea ambako hakuna sekretarieti?"
Pamoja na hayo Mbowe ameongeza kwa kutoa tamko kwamba "Hatutakuwa na hotuba za upinzani katika Bunge hili la Bajeti hadi pale watakaporuhusu kuajiri. Hatutakubali hotuba zetu kuhaririwa"