F Chadema yazungumzia hali ya Halima, yapeleka Daktari | Muungwana BLOG
https://c2p.cleverwebserver.com/dashboard/6a0bec4b-79ba-11ef-ad2b-06f0639468d1

Chadema yazungumzia hali ya Halima, yapeleka Daktari


Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimesema kimeamua kumpelekea daktari wa Mbunge wa Kawe, Halima Mdee ili aweze kumcheki na kuwathibitishia Jeshi la Polisi kuwa Halima ni mgonjwa na wala hakuwa na nia ya kukimbia kuripoti Polisi.

Hayo yamebainishwa na Mkurugenzi wa Itifaki na Mawasiliano ya Mambo ya Nje wa Chadema, John Mrema wakati alipokuwa anazungumza na mwandishi wa habari hii muda mchache alipokamatwa Halima Mdee na Jeshi la Polisi katika uwanja wa ndege wa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere Jijini Dar es Salaam leo (Aprili Mosi, 2018).

"Halima Mdee bado anashikiliwa na Jeshi la Polisi wa kituo cha 'Centro' Jijini Dar es Salaam mpaka hivi sasa japokuwa amewaeleza ukweli kwamba ametoka kwenye matibabu na kuwaonesha vyeti vyote vya hospitali lakini bado wanaendelea kumshikiria", amesema Mrema

Pamoja na hayo, Mrema ameendelea kwa kusema "mpaka sasa hivi hatua tulizozichukua ni kumpeleka daktari wake ili aende kumcheki na kuwathibitishia Polisi kuwa Halima kweli ni mgonjwa pia wanasheria wa chama wataelekea kituoni hapo muda si mrefu".

Halima Mdee ni miongoni mwa viongozi wa Chadema wanaotuhumiwa na Jeshi la Polisi kufanya maandamano yasiyokuwa na kibali kipindi cha uchaguzi mdogo wa marudio katika jimbo la Kinondoni.