F Kamati kuamua rufaa ya Wambura | Muungwana BLOG
https://c2p.cleverwebserver.com/dashboard/6a0bec4b-79ba-11ef-ad2b-06f0639468d1

Kamati kuamua rufaa ya Wambura

RUFAA ya aliyekuwa Makamu wa Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Michael Richard Wambura, sasa imefikia patamu baada ya juzi Jumamosi kusikilizwa katika makao makuu ya shirikisho hilo, Karume jijini Dar es Salaam na hivi sasa watu wengi wanataka kujua nini kinachofuatia.

Hivi karibuni, Wambura alikata rufaa Kamati ya Rufaa ya Maadili ya TFF kupinga maamuzi ya Kamati ya Maadili ya shirikisho hilo ya kumfungia maisha kujihusisha na soka kwa madai ya kufanya ubadhirifu wa fedha za shirikisho hilo pamoja na makosa mengine.

Wakili wa Wambura, Emmanuel Muga, ameliambia Championi Jumatatu kuwa, kamati hiyo iliziita pande mbili zote zinazochuana katika sakata hilo na kuzisikiliza kwa umakini mkubwa.

Alisema katika kikao hicho, mambo yalienda vizuri, kwa hiyo kinachosubiriwa tu hivi sasa ni maamuzi ya hiyo kamati.

“Kamati imesikiliza kwa umakini utetezi wa Wambura, vilevile TFF nao wakizungumza ya kwao kuhusiana na mustakabali mzima wa kesi hiyo. Kwa hiyo tunachosubiri ni hukumu, “ alisema Muga.

Ofisa Habari wa TFF, Clifford Ndimbo alipoulizwa kuwa ni lini hukumu hiyo itatolewa, alisema: “Itakapokuwa tayari basi itatolewa, kwa hiyo wapenzi wa soka waendelee kuwa wavumilivu.”