Wakati kikosi cha Yanga kikielekea Morogoro kwa ajili ya maandalizi ya mchezo wa Kombe la Shirikisho dhidi ya Singida United, Kocha George Lwandamina inaelezwa hakuwa nchini.
Taarifa za ndani zinaeleza kuwa Kocha huyo alisafiri kuelekea Ethiopia kwa ajili ya kuwafuatilia wapinzani wao Welayta Dicha FC waliopangiwa kucheza nao kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika.
Yanga iliondoka mwanzoni mwa wiki hii kwenda Morogoro kuweka kambi maalum ya muda mfupi bila Lwandamina na mpaka wanawasili Singida jana, Kocha huyo alikuwa hajajiunga na kikosi.
Lwandamina amejiunga na kikosi cha Yanga asubuhi ya leo baada ya kuwasili nchini akitokea Ethiopia na kuungana na kikosi mjini Singida.
Hata hivyo ujio wake ndani ya kikosi haujaleta manufaa baada ya Yanga kupoteza mchezo wa Kombe la Shirikisho dhidi ya Singida kwa jumla ya matuta 4-2 baada ya dakika 90 kumalizika kwa sare ya 1-1.