Marekani na Korea Kusini kwa pamoja yameanza mazoezi yao ya kijeshi ya kila mwaka, baada ya zoezi hilo kucheleweshwa kwa karibu mwezi mzima.
Mazoezi hayo yalisitishwa ili kutoa fursa kulegezwa kwa masharti ya mazungumzo kati ya Korea zote mbili, wakati wa mashindano yaliyomalizika ya Olimpiki majira ya baridi.
Katika siku za nyuma, Korea Kaskazini, ilielezea mazoezi hayo ya kijeshi, kama maandalizi ya kuivamia.
Lakini mwandishi wa BBC anasema kuwa, mara hii Pyongyang, imekimya kuhusiana na mazoezi hayo.
Rais wa Korea Kaskazini Kim Jong-un, anasemekana kuwaambia maafisa wakuu wa nchi jirani ya Korea Kusini, ambao walizuru taifa lake kuwa, anaelewa kuwa hali inafaa kusonga mbele.
Mwisho wa mwezi huu, mkutano mkuu umeandaliwa kati ya mataifa hayo mawili, ambayo zamani yalikuwa mahasimu, na utakuwa mkutano wa kwanza kabisa katika kipindi cha muongo mmoja uliopita.