Mufti wa Tanzania athibitisha kufanyika kwa mabadiliko BAKWATA

Mufti wa Tanzania Sheikh Abubakari Zuberi amesema Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA) limefanya mabadiliko ya upatikanaji wa viongozi kwa nchi nzima kuanzia ngazi ya Masheikh wa wilaya, mikoa na Taifa.

Akizungumza leo Jijini Dar es Salaam wakati akitoa maazimio ya kikao cha Baraza Kuu la BAKWATA kikao kilichokaa Mjini Dodoma mwishoni mwa mwezi Machi, Mufti amesema wamekubaliana kwa kauli moja kuwa upatikanaji wa viongozi wa Kiislamu utakua ni wakuteuliwa na sio kuchaguliwa tena kama ilivyo sasa.

Amesema Mkutano Mkuu uliofanyika tarehe Machi 31 - Aprili 1 umesema kuwa mfumo wa uchaguzi hauwaachi watu salama sana sana husababisha migogoro ya hapa na pale na makundi yenye kuleta chuki na kwamba mfumo wa kuteua ndiyo mfumo wa kiislam

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Halmashauri Kuu ya BAKWATA taifa Sheikh Khamis Mataka amesema mbali na utaratibu huo wameanzisha mfumo mmoja wa kukusanya mapato ili kukusanya fedha hizo kwa umakini tofauti na ukusanyaji wa sasa ambao una mapungufu mengi na kupoteza baadhi ya mapato.