Mahakama nchini Kenya imemhukumu afisa wa polisi nchini humo kutumikia kifungo cha miaka 15 jela baada ya kupatikana na hatia ya mauaji ya mwaka 2013 ya mwanaume aliyeshukiwa kuiba simu ya mkononi.
Polisi huyo, Titus Musila alikutwa na hatia ya kumpiga risasi tatu za kichwani mtuhumiwa Kenneth Mwangi badala ya kumkamata.
Wakati akitoa uamuzi huo, Jaji wa Mahakama Kuu James Wakiaga amesema kuwa uamuzi huo ni onyo kwa maafisa wa usalama wanaotumia silaha vibaya.
Kwa mujibu wa wachambuzi Polisi wa Kenya wamekuwa wakilaumiwa na mashirika ya kutetea haki za binadamu pamoja na raia kutokana na mauaji ya kiholela lakini mara nyingi wamekuwa hawachukuliwi hatua au kufunguliwa mashtaka.