Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli leo Aprili 01, 2018 ameungana na wakristo wote katika maadhimisho ya Misa Takatifu ya sikukuu ya Pasaka iliyofanyika katika Kanisa la Mtakatifu Joseph, Jimbo Kuu la Dar es Salaam.
Akizungumza baada ya kukaribishwa na Padre Tegete kutoa salamu, Rais Magufuli amewatakia watanzania wote heri ya Pasaka na ametoa wito kwa watanzania kuendelea kuishi kwa amani na upendo huku wakishiriki ipasavyo katika ujenzi wa Taifa.
"Kifo na ufufuko wa bwana wetu Yesu Kristo ukafufue matendo yetu, tuendelee kuijenga amani yetu, upendo wetu na tujenge maendeleo ya watanzania wote, kwani Kristo alifundisha upendo miongoni mwetu. Kwa hiyo Baba nakushukuru sana kwa kuongoza Misa hii, naomba ufikishe shukrani zangu kwa Kardinali Pengo, Maaskofu wote na watanzania wote tuendelee kusimama pamoja ili kulijenga Taifa letu", amesema Rais Magufuli.
Kwa upande mwingine, Rais Magufuli aliongozana na Mkewe Mama Janeth Magufuli katika Misa hiyo ambayo imeongozwa na Paroko Msaidizi wa Parokia ya Mtakatifu Joseph Padre Venance Tegete.