Serikali ya Tanzania inajiandaa kukata miti eneo la ukubwa wa asilimia tatu ya hifadhi ya taifa Selous.
Mapema asubuhi ya Jumatano, serikali ilipokea maombi ya zabuni ya kukata miti hiyo kutoka kwa makampuni ya ndani na nje ya nchi yaliyoonyesha nia ya kutekeleza mradi huo wa kukata miti.
Serikali inasema ukataji huu wa miti zaidi ya milioni 2 ni maandalizi ya ujenzi wa mradi mkubwa wa bwawa la kuzalisha umeme wa megawati 2,100 utakaojengwa ndani ya hifadhi hiyo.
Hatua hii inaongeza ukosoaji dhidi ya serikali kutoka kwa wanaharakati wa mazingira ambao tangu serikali kutangaza nia ya kujenga mradi huo wa umeme, wamekuwa wakipinga mradi huo kuwa ni hatari kwa wanyama pori na viumbe wengine waishio katika hifadhi hiyo ya Selous, ambayo inatambuliwa pia kama urithi wa dunia.
Wanamazingira watoa tahadhari kuhusu mpango wa serikali
Ni wazi kwamba serikali ya Tanzania imedhamiria kuendelea na mradi huu wa kufua umeme, huku kukiwa na ukosoaji kutoka kwa wanaharakati wa mazingira, ambao wanaelezea wasiwasi wao kuhusiana na athari za hali ya mfumo wa kiikolojia ndani ya hifadhi ya Selous.
Hata hivyo hivi karibuni kuhusu mradi huo Rais John Magufuli aliweka wazi kwamba, serikali yake haitakwamishwa na ukosoaji wa aina yoyote ya kimazingira katika kutekeleza mradi huu mkubwa wa umeme.
Rais alisistiza kuwa wakati serikali yake inatekeleza sera ya viwanda,mradi huu wa umeme,ni muhimu zaidi kufikia malengo hayo.
Mtendaji mkuu wa wakala wa misitu Tanzania Profesa Dosantos Silayo ameiambia BBC sababu za kuuzwa kwa miti itakayo katwa kwenye hifadhi hiyo kupisha mradi huo.
''Sasa serikali imeona si vizuri kuiondoa miti katika hali ya kuiharibu inaweza kuwa na thamani, serikali imeamua kuitoa kwa utaratibu ambao utaiwezesha iuzwe kwenye makampuni mbalimbali kwa ajili ya matumizi ya kutengeneza samani ndani na nje ya nchi, hii si biashara, na kwa kweli haijawa nia ya serikali kufanya uharibifu kwenye hifadhi zake''.