F Ashikiliwa na Polisi kwa tuhuma za kumuua mwanae kwa kumchapa na fimbo | Muungwana BLOG
https://c2p.cleverwebserver.com/dashboard/6a0bec4b-79ba-11ef-ad2b-06f0639468d1

Ashikiliwa na Polisi kwa tuhuma za kumuua mwanae kwa kumchapa na fimbo


Jeshi la Polisi katika Wilaya ya Pader, nchini Uganda, linamshikilia Bwana Omony Odokonyero (30) kwa tuhuma za kusababisha kifo cha mwanae mwenye umri wa miaka saba kilichotokana na kuchapwa  fimbo.

Kwa mujibu wa gazeti la Daily Monitor limeripoti Juni 7 2018, katika kijiji cha Omakigira, ambapo mtoto huyo aliyejulikana kwa jina la Richard Odokonyero, mwanafunzi wa shule ya msingi Pader Ogom alipigwa na fimbo baada ya kukataa kwenda shule akitaka kupelekwa kwa bibi yake.

Mwenyekiti wa Kijiji hicho Charles Lalobo, amethibitisha tukio hilo na kudai kuwa mzazi huyo amekuwa na tabia ya kumpiga mtoto wake mara kwa mara na siku ya tukio alikuwa akimpiga na fimbo kichwani  hivyo kupelekea kuzimia kabla ya kufariki

“Hili ni tukio ambalo halikupaswa kutokea, kuna njia nyingi za kutumia kama mzazi ili kufundisha watoto wao lakini sio kutoa athabu kali, Polisi wanapaswa kuchukua hatua kali na kuhakikisha mtuhumiwa anaadhibiwa” amesema Bwana Lalobo

Msemaji wa Jeshi la Polisi katika mkoa wa Aswa River, Jimmy Okema, amesema kuwa Jeshi hilo linamshikilia mtuhumiwa katika Makao Makuu ya Polisi Pader na kuongeza kuwa endapo uchunguzi ukikamilika atafikishwa mahakamani kwa kosa la mauji.