Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata) limewatoa hofu Waislamu wote ambao wanatarajia kwenda kufanya ibada ya Hijja, likieleza kuwa limejipanga kuhakikisha usumbufu uliojitokeza mwaka jana haujirudi.
Mwenyekiti wa baraza hilo, Sheikh Hamisi Mataka alisema jana kuwa: “Taasisi nne ambazo ni Tanzania Charitable Oraganization, Hajj Hikma, Taqwa Hajj Group na Almadina Social Services Trust hazitosafirisha mahujaji kwa kuwa hazijakidhi masharti yaliyowekwa. Hatutaki mambo yaliyojitokeza mwaka jana, yajirudie sasa.”
Mataka ameeleza hayo katika mkutano na waandishi wa habari na kuongeza kuwa zaidi ya mahujaji 100 mwaka, 2017 walikwama kwenda kwenye ibada hiyo baada ya taasisi ya moja iliyokusanya fedha zao kwa madai ya kuwawezesha kusafiri, kuingia mitini.
“Mpaka sasa mambo yote yanakwenda vizuri, hakuna tishio lolote ambalo tumelibani la mahujaji kutosafiri kwa sababu mambo yote yapo katika mstari kuhakikisha kuwa Waislamu wanatekeleza ibada hiyo,” alisema Mataka.
Mataka alisema taasisi 11 pekee ndizo zilizokidhi vigezo na msharti yaliyowekwa ikiwamo , Alhusna Hajj Trust, Shamsul Maarifa Kheri na Tanzania Muslim Development Asociatiaon na Tanzania Muslim Hajj Trust.