F Dk.Kigwangalla atoa siku 30 waliovamia Pori la Swagaswaga | Muungwana BLOG
https://c2p.cleverwebserver.com/dashboard/6a0bec4b-79ba-11ef-ad2b-06f0639468d1

Dk.Kigwangalla atoa siku 30 waliovamia Pori la Swagaswaga


Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla ametoa siku 30 kwa wananchi waliovamia Pori la Akiba Swagaswaga na kuendesha shughuli zao ikiwemo kilimo, makazi na ufugaji ndani ya pori hilo kinyume cha Sheria waondoke mara moja kwa hiari yao kabla ya kuondolewa kwa nguvu.

Ametoa agizo hilo jana kwenye mkutano wa hadhara katika kijiji cha Handa Wilaya ya Chemba mkoani Dodoma wakati wa ziara yake ya kikazi ya kutatua mgogoro wa ardhi kwenye hifadhi hiyo wilayani humo.

"Tunawapa siku 30 muanze kutoka wenyewe, baada ya siku 30 tunatoa notisi ya siku nyingine 30 za kutumia nguvu, kwahiyo kuanzia sasa hivi anzeni kujipanga wenyewe na kuondoka wakati Halmashauri ikifanya tathmini ya maeneo ya vijiji ambavyo ni halali ya kuwagawia kwa wale watakaopenda kupewa maeneo huko", alisisitiza Dk. Kigwangalla.

Alisema sheria za uhifadhi haziruhusu mtu yeyote kuingia ndani ya maeneo ya hifadhi na kuendesha shughuli za kibinadamu na kwamba kufanya hivyo ni kudharau Sheria na Malmlaka zilizopo.

Alisema kwa upande wa wananchi wa kijiji cha Handa ambacho kilianzishwa kimakosa ndani ya pori hilo wataendelea kubaki mpaka pale wizara yake kwa kushirikiana na Wizara ya Tamisemi na Ardhi zitakapoamua hatma yao ikiwemo ama kulipwa fidia kupisha eneo hilo au waendelee kubaki na mipaka ya hifadhi isogezwe.

Katika hatua nyingine, Dk. Kigwangalla ameiagiza Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania TAWA kujenga miundombinu ya kuvuta maji kutoka katika chemchem iliyopo ndani ya hifadhi hiyo na kuyasogeza kwenye makazi ya wananchi ili kulinda chanzo hicho kwa kuzuia uharibifu unaofanywa na wananchi wanaofuata huduma katika eneo hilo.