Katibu Mkuu wa UWT aahidi makubwa CCM


Katibu Mkuu wa Umoja wa wanawake wa Chama Cha Mapinduzi Tanzania (UWT), Ndugu Queen Mlozi ameahidi kufanya kazi kwa weledi, uaminifu na uzalendo uliotukuka ili CCM ishinde katika uchaguzi mkuu wa dola mwaka 2020.

Hayo ameyasema wakati akizungumza na viongozi na watendaji wa ngazi mbali mbali za UWT Zanzibar hapo Afisi Kuu CCM Kisiwandui katika ziara yake ya kwanza kujitambulisha kwa viongozi na watendaji hao.

Alisema atatekeleza majukumu yake kwa ufanisi kwa lengo la kuimarisha taasisi hiyo ili kwenda sambamba na kasi ya maendeleo ndani ya Umoja huo na Chama kwa ujumla.Ameeleza kwamba wanawake wa UWT wanatakiwa kuelekeza nguvu zao katika kulinda maslahi ya CCM ili ishinde kwa ngazi zote kwa upande wa Tanzania bara na Zanzibar katika uchaguzi Mkuu ujao.

Katibu Mkuu huyo amewashukuru viongozi viongozi wote wa Chama Cha Mapinduzi waliomuamini na kumteuwa kushika nafasi hiyo ya ngazi ya juu ya kiutendaji kupitia Kikao cha Halmashauri Kuu ya CCM Taifa (NEC) kilichofanyika hivi karibuni Jijini Dar es saalam.

“ Viongozi na wanachama wote nakuahidini kwamba nitatumia weledi na uzoefu wangu wote kwa kuhakikisha UWT inaendelea kuwa imara na mkombozi na mtetezi mkubwa wa maslahi ya wanawake wote nchini”, alisema Queen.Akizungumza Mwenyekiti wa UWT Taifa, Ndugu Gaudencia Kabaka alisema ushirikiano anaoupata kutoka kwa viongozi mbali mbali wa Umoja huo na Chama unampa nguvu na imani ya kusimamia maslahi ya taasisi hiyo bila hofu.