Kocha wa Uholanzi awalipa wachezaji mishahara


Kocha wa timu ya taifa ya Australia Bert van Marwijk, ameamua kuwalipa mishahara makocha wenzake kwenye benchi la ufundi la timu hiyo, ambayo imefuzu kucheza fainali za Kombe la Dunia 2018 nchini Urusi.

Marwijk ambaye ni raia wa Uholanzi amefikia uamzi huo baada ya chama cha soka nchini humo kumgomea kumpa bajeti ya kuongeza wataalam kwenye benchi lake kutokana na ukosefu wa pesa za kuwalipa makocha hao.

Hata hivyo yeye amedai ameamua kufanya hivyo kwasababu anataka timu ifanye vizuri na hivyo ndio taaluma yake inamtaka afanye, bila kujali malipo huku akiongeza kuwa hata hao aliowachukua wanajali zaidi suala la taaluma na sio malipo.

''Kwenye kitu chochote kinachohitaji mafanikio hususani kwenye taaluma lazima malipo yawe kitu cha mwisho lakini weledi uanze mwanzo na ndio kinafanyika hapa, tunataka tufanye vizuri Urusi na hiyo itatupa fursa nyingi sisi'', amesema.

Van Marwijk aliteuliwa kuwa kocha wa muda wa timu hiyo  mapema mwezi Januari kufuatia kujiuzulu kwa Ange Postecoglou, ambaye aliiongoza Australia kufuzu fainali hizo. Australia ipo kundi C na timu za Ufaransa, Denimark na Peru.