Serikali yaingilia kati suala la Mwanamke kujifungulia nje ya Kituo cha Polisi


Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani, Hamad Masauni amesema hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi ya askari polisi waliosababisha mwanamama Amina Rafael kujifungua nje ya kituo cha Polisi cha Mang’ula huko mkoani Morogoro.

Kauli hiyo ya Masauni imekuja baada ya kutakiwa kutoa maelezo na Mwenyekiti wa Bunge, Andrew Chenge kuhusiana na madai hayo yaliyotolewa na Mbunge wa Arumeru Mashariki , Joshua Nassari aliyetaka suala hilo lijadiliwe ndani ya Bunge na kwamba ni matukio yanayoendelea kujitokeza ikiwamo Dar es Salaam, Tarime na Mwanza.

Naibu Waziri Masauni amesema, serikali imesikitishwa na suala hilo na tayari jalada la uchunguzi limeshafunguliwa.

Akielezea tukio hilo Masauni amesema "kulikuwa na tukio la wizi, lililomhusisha mume wa huyu mama, (Abdallah Mohamed), anayedaiwa kununua vitu vya wizi ambavyo vilikutwa katika nyumba yake, Polisi walimtaarifu mama kwamba mume wake atakaporejea afike polisi. Lakini hakufika na polisi walimchukua yule mama kwenda kumhoji,".

Pamoja na hayo amesauni amweka wazi kuwa busara ingewez kutokana na hali y mwanamama huyo na kwamba angehojiwa kisha kuachiwa.

Sanjari na hayo leo wakati akizungumza na wanahabari jijini Dar es salaam, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dkt. Mwigulu Nchemba amesema kuwa bado suala hilo linafuatiliwa ili kujua ukweli wa jambo.