WAZIRI wa Afya Hamad Rashid Mohammed amesema huduma za kitengo cha usafishaji figo kwa wagonjwa wenye matatizo hayo katika Hospitali ya Mnazi Mmoja zinaendelea kufanyika bila ya malipo yeyote .
Hayo aliyasema huko katika Hospitali ya Mnazi Mmoja wakati alipokuwa akifanya ziara ya kukagua kitengo hicho na kuona jinsi kinavyoendelea na huduma zake zinazofanyika katika sehemu hiyo kwa kuhudumia wagonjwa kama kawaida.
Alisema lengo la ziara hiyo ni kuona jinsi wananchi wanavyofaidika na huduma hiyo kwani Serikali inataka wananchi wake wasihangaike kutafuta huduma hiyo kwa kuifuata nje ya nchi au masafa marefu.
Aidha alisema Serikali kupitia Wizara ya Afya kwa kuwajali wananchi wake imekuwa iko imara katika kuhakikisha inakipa kipaumbele kwa kukipatia vifaa vyote pamoja na dawa za kusafishia mafigo.
“Wananchi mnapofikwa na matatizo haraka fikeni Hospitalini ili muweze kupata huduma dawa zipo za kutosha na madaktari wapo , na Serikali inataka wananchi wenye afya ili waweze kujenga Taifa lililo bora”alisema Waziri huyo.
Pia alifahamisha kuwa atahakikisha anazitatua changamoto zinazozikabili Hospitali hiyo kwa sababu ndio tegemeo kubwa kwa wananchi walio wengi na wasio na uwezo wa kwenda kujitibu nje ya nchi.
Vile vile akiendelea na ziara yake alifika wodi ya wazazi na alisema atalifanyia ufumbuzi suala la msongamano kwa lengo la kupunguza wazazi wanaojifungulia Hospitali hiyo, kwa kufungua wodi iliyokuwa ya zamani baada ya kukamilika kwa matengenezo yake.
Nae Mkurugenzi wa uendeshaji waUtumishi wa wizara hiyo Ramadhani Khamis amewataka baadhi ya wazazi waliokuwa hawana matatizo makubwa wanapotaka kujifungua wafike kwenye vituo vya karibu kama vile Fuoni, Chumbuni Sebleni ili kuweza kupunguza msongamano huo.
Akitoa wito kwa wananchi alisema iwapo watatozwa pesa za dawa wasiogope kutoa ripoti ili hatua za sheria ziweze kufanya kazi zake, muhimu watoe ushahidi wa uhakika kwani dawa zipo za kutosha.
Sambamba na hayo Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali hiyo Ali Salim amewaasa madereva kuwa makini wanapokuwa bararani kwani ajali zimekuwa nyingi na zinapunguza nguvu kazi kwa taifa baada ya wananchi kuvunjika viungo au kufariki.