F ‘Dada poa’ wadakwa kwa kuwauzia ngono Wanafunzi sekondari | Muungwana BLOG
https://c2p.cleverwebserver.com/dashboard/6a0bec4b-79ba-11ef-ad2b-06f0639468d1

‘Dada poa’ wadakwa kwa kuwauzia ngono Wanafunzi sekondari


JESHI la Polisi mkoani Katavi limewakamata wanawake 14 wanaodaiwa kufanya biashara ya kuuza miili yao maarufu ‘madadapoa’, ambao inadaiwa wateja wao wakubwa wakiwa wanafunzi wa kiume wa sekondari.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Katavi, Damas Nyanda, alisema watuhumiwa hao walikamatwa juzi usiku kufuatia msako uliofanyika katika Mtaa wa Majengo maarufu ‘Mtaa wa Fisi’ katika Mji wa Mpanda Manispaa ya Mpanda, huku akisisitiza msako huo ni endelevu.

Alibainisha kuwa msako huo ulifanyika katika madanguro matano na nyumba ya kulala wageni jirani na kituo cha mafuta cha Allyen katika Mji wa Mpanda.

Kamanda Nyanda alieleza kuwa madada hao kabla ya kupelekwa mahakamani, watachukuliwa alama za vidole vyao na kupigwa picha.

Alisema msako huo umefanywa kufuatia malalamiko ya wazazi kuwa wanafunzi wa kiume wa sekondari ni miongoni mwa wateja wa uhakika wa ‘madadapoa’ hao, huku wakionyesha wasiwasi wao wa uwezekano wa kupata maambukizi ya Virusi Vya Ukimwi (VVU).

Taarifa za uhakika zinaeleza wengi wa ‘madadapoa’ hao wanatoka mikoa ya Tabora, Kigoma, Mbeya, Rukwa, Singida, Manyara, Arusha, Dodoma na mikoa ya Kanda ya Ziwa.

Inadaiwa kuwa ‘dadapoa’ hao awali walikuwa wakifanya biashara hiyo ya kuuza miili yao katika machimbo ya madini ya dhahabu ya Isumamilolo mkoani Katavi, lakini baada ya dhahabu kupungua na biashara yao kudorora, waliamua kuvamia Mtaa wa Fisi na kuendelea na biashara ya kuuza miili yao.

Baadhi yao ambao wamenusurika kukamatwa wakati wa msako huo,  kwa masharti ya majina yao kutoandikwa gazetini, walikiri kuwa wamepanga nyumba yote ambapo wanamlipa mmiliki nyumba Shilingi 6,000 kila siku kwa kila chumba, hivyo kwa mwezi kila chumba kinalipiwa Shilingi 180,000.

“Biashara ni nzuri inalipa sana kwani katika siku nzuri napata na kuwahudumia kingono wateja kati ya kumi hadi kumi na watano … wateja wetu wa kubwa ni wanafunzi wa sekondari na vijana wa kiume ambao wanachangamsha sana biashara,” alibainisha mmoja wao.

Aidha, walibainisha kuwa biashara hiyo inachangamka sana siku za mwisho wa wiki ambapo mteja analipia huduma hiyo kwa shilingi 5,000 kwa muda mfupi, huku mteja anayetaka huduma usiku kucha anatakiwa kulipa shilingi 20,000.

“Wanaume wa Mpanda wengi wao ni wakarimu na sio wabahili katika kulipa fedha kadri mtakavyokubaliana, tofauti na wa mikoa mingine niliyowahi kutembelea,” alieleza ‘dadapoa’ mwingine.

Kwa upande wao, wakazi wa Mtaa wa Fisi walidai kuwa biashara hiyo ni hatarishi pia kwa watoto wao wa kiume na wa kike, huku wakibainisha kuwa ifikapo saa 2:00 usiku, makundi ya vijana wa kiume humiminika kwenye mtaa huo wakiwasaka ‘madadapoa hao.

Diwani wa Kata ya Majengo, Willy Mbogo ambaye ni Meya wa Manispaa ya Mpanda, anakiri kupokea malalamiko ya wakazi wa Mtaa wa Fisi na kwamba alisharipoti katika Kituo cha Polisi mjini Mpanda.

Kwa mujibu wa Mbogo, alihakikishiwa na jeshi hilo kuwa watafanya msako wa kuwaondoa ‘dadapoa’ hao mtaani hapo.

“Sifurahishwi kabisa na biashara hii inayofanywa kwenye kata yangu, ukizingatia pia mimi naishi jirani na Mtaa wa Fisi,” alisema Mbogo.