KAIMU Balozi wa Marekani nchini, Inmi Patterson, ameahidi serikali yake kutoa ushirikiano katika ujenzi wa shule za msingi na sekondari katika jimbo la Rufiji ili kupunguza idadi ya wanafunzi ambao wanashindwa kusoma kutokana na ukosefu wa shule.
Dk Patterson,aliyasema hayo jana wakati wa ziara yake ya kukagua shule zilizopo katika jimbo hilo ambapo alishuhudia wanafunzi wakisoma katika majengo yaliyoezekwa na makuti huku shule ikiwa na darasa moja ambalo linabeba zaidi wanafunzi 150.
Katika ziara hiyo ambayo Dk.Patterson,aliongozana na Mbunge wa jimbo hilo, Mohamed Mchengerwa, (CCM) alifika katika kijiji cha Ngalo na kushuhudia wanafunzi wakisoma kwa kukaa chini kutokana na kukosa viti na madarasa jambo ambalo lilimfanya aahidi kuwa serikali yake itasaidia katika kuboresha miundombinu ya jimbo hilo.
Hata hivyo kiongozi huyo pia alishuhudia watoto wa kijiji cha Mtanange wakiwa hawasomi kabisa kutokana na kukosekana kwa shule hivyo asilimia 90 ya wananchi wa kitongoji hicho hawajui kusoma na kuandika.
"Tutajitahidi kuwasaidia katika elimu kwa kadri tutakavyoweza, nimejionea hali halisi ni kweli kuna changamoto na naamini kuwa ukiwasaidia watu katika elimu ni moja ya njia ya kuwaokoa kwani wakielimika watapambana kuujenga uchumi wa kwao "alisema Dk Patterson
Kwa upande wake Mchengerwa aliushukuru ubalozi huo kwa kuonyesha nia ya kusaidia katika elimu jimboni hapo na kueleza kuwa msaada huo utasaidia kupunguza kundi kubwa la watoto wanaokwenda kulima kutokana na kukosekana kwa shule.
"Nashukuru marafiki zetu Marekani kwa kuitikia ombi langu nililolitumia kwenu naamini kuja kwenu hapa kutakuwa manufaa makubwa kwetu, nimeomba kusaidiwa ujenzi wa shule ambazo zitaweza kustahimili mafuriko (mobile school) "alisema Mchengerwa
Naye Mwenyekiti wa kitongoji cha Njogolo,Ramadhani Ngalanga, alionesha kufurahishwa na ujio wa balozi huyo akieleza kuwa inaweza ikawa njia ya ukombozi kwa watoto wa kitongoji hicho pamoja na jimbo lote la Rufiji ambao wanaoshia kulima na kuolewa bila kupata elimu ambayo ni haki yao ya msingi.