F Peter Msigwa: Hakuna wa kunizuia nikitaka kumpongeza Rais | Muungwana BLOG
https://c2p.cleverwebserver.com/dashboard/6a0bec4b-79ba-11ef-ad2b-06f0639468d1

Peter Msigwa: Hakuna wa kunizuia nikitaka kumpongeza Rais


Mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa (CHADEMA) ameweka bayana kwamba hahitaji kuviziwa na mtu yoyote katika suala la kusifu utendaji wa Rais Magufuli pamoja na serikali yake kwani ana uwezo wa kununua kipindi katika televisheni ili kuweza kufanya jambo hilo.

Akifanya mahojiano na www.eatv.tv, Msigwa amesema kwamba kitendo cha kusambaa kwa kipande cha 'video' kilichokuwa kikimuonyesha akimsifu Rais wakati alipokuwa kwenye ziara mkoani Iringa kilikuwa cha kuviziwa na
kilikuwa na lengo la kumchafua kisiasa.

Mbunge huyo wa upinzani amedai kwamba kitendo cha hali ya uchumi wa nchi kuwa mdogo, watu kuokotwa kwenye viroba na demokrasia kukandamizwa ndivyo vinamfanya kushindwa kutoa pongezi lakini siku akiona inahitajika, atafanya hivyo na siyo kuviziwa viziwa kama jinsi ilivyofanyika awali kupitia kipande cha 'video'.

"Hakuna wa kunizuia nikitaka kumpongeza Rais, hivyo sihitaji kuviziwa.  Mimi sikumpongeza Rais ile siku na simpongezi. Kilichofanyika naweza kusema 'I was taken out of context' Nina uwezo wa kununua kipindi ili kumsifia Rais ila si kwa kuviziwa viziwa," amesema Msigwa.

Akizungumzia kuhusu wakati mgumu alioupata ndani ya Chama chake na kwa wafuasi wanaoiunga mkono CHADEMA baada ya kusambaa kwa 'video' ile, Msigwa amesema haikuwa rahisi kueleweka na watu wote.

"Chama changu kinajua msimamo wangu, hivyo niliwaeleza wakanielewa. Watu wengine haikuwa rahisi  kunielewa kutokana na kale ka video cha sekunde 53 ambacho kalikatwa mwanzo na mwisho. Wasomi na watu wanaoniamini walielewa," ameongeza Mch. Msigwa.

Rais Magufuli akiwa katika ziara yake ya kikazi mkoani Iringa, Mei 3, mwaka huu wakati kulisambaa 'video' inayomuonyesha Mch. Msigwa akimsifia Rais, ambapo kwa mujibu wake amesema ni kama aliviziwa kwani hata walipoingia ndani kuzungumza na Rais hawakuwa na vifaa vyao vya mawasiliano zaidi ya waandishi wa Ikulu.