F Pombe za kienyeji kutumika kuua wadudu wanaoharibu Kahawa | Muungwana BLOG
https://c2p.cleverwebserver.com/dashboard/6a0bec4b-79ba-11ef-ad2b-06f0639468d1

Pombe za kienyeji kutumika kuua wadudu wanaoharibu Kahawa


Na Ferdinand Shayo,Kilimanjaro
Pombe za kienyeji aina ya Mbege,Dengelua  na Rubisi zimegundulika na Watafiti kuwa harufu yake inaweza kutumika kuua wadudu aina ya Ruhuka wanaofahamika kitaalamu kama Cofee berry borrer ambao hutoboa matunda ya kahawa na kupunguza mazao ya mkulima hivyo kusababisha hasara.

Mtafiti katika Programu ya kuongeza tija na Ubora wa Kahawa kutoka taasisi ya Utafiti wa Kahawa  Tanzania (TACRI) ,Suzan Mbwambo alisema kuwa wadudu hao wamekua wakiwasumbua wakulima hivyo wamebaini njia za kukabiliana na wadudu hao kwa kutumia vitu vinavyopatikana kirahisi katika maeneo yanayowazunguka ikiwemo pombe za kienyeji.

Suzan alisema kuwa Wakulima wanaweza kutumia vilevi kama Mbege na Dengelua na nyinginezo kuziweka katika chupa na kuzining`iniza mashambani kwa harufu yake inaua wadadu hao wanaoshambulia matunda ya kahawa na kuyatoboa.

Akizungumza katika Ziara ya Naibu Waziri wa Kilimo ,Mtafiti huyo alisema kuwa kwa sasa wanaendelea kufanya tafiti mbalimbali zitakazowasaidia wakulima kupambana na wadudu wanaoharibu kahawa pamoja na magonjwa ya kahawa ili kukuza kilimo hicho pamoja na kuinua kipato cha wakulima.

Naibu Waziri wa Kilimo Omari Mgumba alisema kuwa taasisi hiyo inapaswa kupeleka tafiti wanazozifanya kwa wakulima ili ziweze kuwasaidia na kuboresha kilimo chao ili waweze kulima kilimo cha kisasa na kuondokana na umasikini.

Alisema kuwa Taasisi hiyo ina jukumu la kuhakikisha kuwa linafanya tafiti za kuongeza tija kwenye kilimo ikiwa ni pamoja na kutafiti dawa za kusaidia kukabiliana na wadudu waharibifu wanaoharibu kahawa.